Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb.), na Waziri wa Masuala ya Shirikisho, Ulaya na Kimataifa wa Ujerumani, Mhe. Manfred Pentz, wamejadili fursa za kuimarisha biashara na uwekezaji. Majadiliano hayo yamefanyika Septemba 16, 2026 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa Invest EastAfrica uliohusisha makampuni 30 ya Ujerumani.
Akizungumza katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Balozi wa Ujerumani nchini, Mhe. Annet Günther, alieleza kuwa Ujerumani inalenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Alisisitiza kuwa Tanzania ina nafasi ya pekee ya kukuza uhusiano wa kiuchumi na kufungua fursa mpya kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Mhe. Judith Kapinga alisema Serikali imejikita katika kupanua fursa za biashara na viwanda kimataifa. Alifafanua kuwa jitihada hizo ni pamoja na kupunguza vikwazo vya kibiashara ili kuwezesha sekta binafsi ya pande zote mbili kunufaika kikamilifu.
Naye Mhe. Manfred Pentz alieleza kuwa Ujerumani inaamini katika kujenga ushirikiano imara na wa muda mrefu na Tanzania pamoja na Afrika Mashariki. Alisisitiza umuhimu wa kugeuza mazungumzo hayo kuwa hatua za vitendo za utekelezaji wa miradi ya kiuchumi.

