Baadhi ya Madereva kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) wakiwa katika picha ya pamoja siku ya tano (Septemba 16, 2026) ya Kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania linaloendelea jijini Dodoma. Kutoka kushoto ni Benard Kiwale, Yohana Kika, Hassan Kijazi na John Jumbe.
🔶 WAAHIDI UTENDAJI MAHIRI ZAIDI
Na WMA – DODOMA.
Baadhi ya madereva kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) wanashiriki Kongamano la Tano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (MST-TGDU) linaloendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Kongamano hilo la kitaifa lililoanza Septemba 12 limewakutanisha mamia ya madereva wa Serikali kutoka mikoa yote nchini, ambapo pamoja na mambo mengine wanajadili mustakabali wa taaluma yao, changamoto wanazokutana nazo barabarani na namna ya kuimarisha nidhamu na weledi kazini.
Kwa mujibu wa waandaaji, kongamano hili ni zaidi ya mkutano wa kawaida; ni darasa huru la kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya za uendeshaji salama, matunzo ya vyombo vya moto vya Serikali na umuhimu wa uwajibikaji katika kulinda mali za umma.
Akizungumza kwa niaba ya madereva wa WMA, Dereva Mkuu kutoka WMA Mkoa wa Dodoma, Bw. John Jumbe amesema ushiriki wao umewapa fursa ya kipekee kujifunza na kuona thamani ya taaluma yao.
 “Tumefurahi sana kushiriki kongamano hili. Tumebadilishana uzoefu na wenzetu kutoka taasisi nyingine na tumejifunza mengi kuhusu uwajibikaji, usalama barabarani na namna ya kuwa mabalozi wazuri wa WMA na Serikali kwa ujumla. Tutaenda kuyafanyia kazi tuliyojifunza,” amesema Bw. Mhando.
Ushiriki wa WMA katika kongamano hilo unaakisi dhamira ya Wakala inayoongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Alban Mark Kihulla, ya kuendelea kuwawezesha watumishi wake katika ngazi zote ili kuhakikisha wanatoa huduma bora na yenye tija kwa wananchi.Â
Kaulimbiu ya Kongamano hilo linalotarajiwa kuhitimishwa Septemba 19, 2026 ni ‘Dereva wa Serikali, Nguvu Moja, Sauti Moja, Kulinda Amani ya Nchi ni Jukumu letu pia.’
Baadhi ya Madereva kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) wakishiriki katika Kongamano la Tano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania, Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Septemba 16, 2026.

