Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema Serikali imeanza kuweka mikakati ya kukabiliana na ongezeko la wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza, ikiwemo kushirikiana na wamiliki wa shule binafsi wakati ujenzi wa shule mpya ukiendelea.
Chalamila amesema mabadiliko ya mfumo wa elimu yamesababisha kuwepo kwa kundi kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu elimu ya msingi na kuingia kidato cha kwanza kwa wakati mmoja, hali inayohitaji maandalizi ya mapema ya miundombinu.
Amesema Mkoa wa Dar es Salaam unaendelea na ujenzi wa shule na madarasa mapya, lakini pamoja na hatua hizo, Serikali imeona umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi ili kuongeza nafasi za wanafunzi katika kipindi cha mpito.
Amesema baadhi ya shule binafsi zilizojengwa miaka iliyopita kwa sasa zina nafasi ambazo hazitumiki kikamilifu kutokana na kupungua kwa idadi ya wanafunzi, hivyo Serikali inatazamia kushirikiana na wamiliki wake kuzitumia kupitia makubaliano maalumu.
Kwa mujibu wa Chalamila, utaratibu huo unaweza kuhusisha Serikali kutumia baadhi ya shule hizo kwa muda maalumu wakati ikiendelea kujenga miundombinu yake, hatua ambayo itasaidia kupunguza msongamano katika shule za Serikali.
Amesema Serikali pia inaendelea na ujenzi wa shule zenye majengo ya ghorofa pamoja na madarasa mapya katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, huku bajeti zilizotengwa kwa sekta ya elimu zikitumika kuongeza uwezo wa kupokea wanafunzi.
Chalamila amesema Mkoa pia umeandaa mpango wa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo wamiliki wa shule binafsi, ili kuhakikisha wanafunzi wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza wanapata nafasi za kusoma bila kuathiri ubora wa elimu.
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo utakuwa wa muda na utalenga kuziba pengo la nafasi za wanafunzi wakati Serikali ikiendelea na ujenzi wa shule na madarasa mapya katika maeneo yenye uhitaji.
Amesema maandalizi hayo yanafanyika mapema ili kuepusha changamoto ya uhaba wa nafasi za wanafunzi na kuhakikisha ongezeko la idadi ya wanafunzi linakwenda sambamba na upatikanaji wa miundombinu na walimu.
