Na: OWM – TAMISEMI, Lindi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Mkandarasi KIKIM Contractors Limited kwa kushirikiana na mbia wake AMACO Enterprises katika Manispaa ya Lindi.

Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 5.3, Stendi ya Mabasi Mitwero, Soko Kuu la Matopeni na Ofisi ya Mradi, inayotekelezwa na Serikali kupitia Mradi wa Ustawishaji Miji Tanzania (TACTIC).

Prof. Shemdoe ameeleza kutoridhishwa kwake na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo Septemba 15, 2026, mara baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Mitwero na Soko Kuu la Matopeni, ambapo alibaini kuwa utekelezaji wake umefikia asilimia 23, huku ikiwa imesalia miezi mitano kabla ya muda wa kukamilisha na kukabidhi miradi hiyo.

Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Prof. Shemdoe amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Kighoma Malima, kuhakikisha suala la utekelezaji wa mikataba hiyo linashughulikiwa kwa mujibu wa masharti ya mikataba, ili kuharakisha utekelezaji na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, hawa wanaotukwamisha ni wakandarasi wazawa ambao usipowapa kazi wanalalamika. Hivyo, Mheshimiwa RC, hawa wana mikataba, shughulikia suala hili kwa mujibu wa mkataba, kwani wakandarasi hawa wanaonekana ni wababaishaji,” amesema Prof. Shemdoe.

Aidha, Prof. Shemdoe amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Lindi kukutana na wakandarasi hao ili wampe mpango mkakati wa kukamilisha miradi hiyo haraka iwezekanavyo, na kuwasilisha kwake mpango kazi huo ifikapo Septemba 23, 2026.Vilevile, ameelekeza kuwa kila baada ya wiki mbili apatiwe mrejesho wa utekelezaji wa mpango huo, ili kufahamu hatua zinazochukuliwa na maendeleo ya miradi hiyo.

Akieleza chanzo cha kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mwakilishi wa Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya Interconsult Ltd, ambaye pia ni Mhandisi Mkazi, Mhandisi Rashidi Abdallah, amesema changamoto hiyo imetokana na mkandarasi kutokuwa amejipanga vyema kiutendaji, kutokuwa na rasilimaliwatu ya kutosha na kutumia vibaya fedha za awali alizolipwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi.

Naye mmoja wa Wakurugenzi wa kampuni zilizopewa kandarasi hizo, John Daniel, amekiri kuwa wamechelewa kutekeleza miradi hiyo kutokana na uzembe, huku akieleza kuwa wamejipanga kufanya kazi usiku na mchana baada ya kuzifanyia kazi changamoto zilizokuwa zikikwamisha utekelezaji. 

Bw. Daniel ameomba kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi ili kuwasilisha mpango kazi wao, huku akimuomba Mkuu wa Mkoa kuwawekea malengo ya muda mfupi yatakayowawezesha kukamilisha kandarasi yao kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema atakutana na wakandarasi hao ili wamueleze mkakati wanaokuja nao wa kukamilisha miradi yote ndani ya miezi mitano iliyobaki.

Mhe. Malima amewataka wakandarasi hao, wakati wa kikao hicho, kuwa tayari kuridhia kutoa mkataba mdogo (sub-contract) kwa mkandarasi mwingine kutekeleza sehemu ya mradi endapo wataona hawana uwezo wa kuikamilisha kwa wakati.

Katika ziara yake ya Septemba 15, 2026, Prof. Shemdoe alitembelea na kukagua pia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Daraja la Ng’uni katika Kata ya Nanganga, ujenzi wa shule mpya ya msingi eneo la Shule ya Sekondari Kitandi, ujenzi wa Kituo cha Afya Chiola Nachingwea, pamoja na kufanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mtuha, Nachingwea DC.