Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linachunguza tukio la mauaji ya kijana aitwaye Steven Karakira Kaaya, (24), Mkazi wa Mtaa wa Boma Mbuzi, Wilaya ya Moshi, ambaye alifariki dunia baada ya kushambuliwa na watu mbalimbali kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa kiti cha plastiki.
Tukio hilo limetokea Septemba 13, 2026, majira ya saa 11:00 jioni, katika eneo la Mtaa wa Spencorn, Kata ya Bomambuzi, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.
Inadaiwa kuwa, wakati wa tukio hilo, kijana huyo alishambuliwa katika sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia kitu butu na watu ambao majina yao yanahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi anbapo hali yake ilizidi kuwa mbaya na hatimaye alifariki dunia.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa mmoja kwa mahojiano zaidi, huku uchunguzi ukiendelea ili kuwabaini na kuwakamata watu wengine wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo.
Aidha, baada ya tukio la mauaji kutokea, baadhi ya wananchi walijichukulia sheria mkononi kwa kufanya vurugu na kusababisha uharibifu wa mali, ikiwemo kuchoma moto gari aina ya Mitsubishi Centa lenye namba za usajili T.119 ATV kwa madai kwamba mmoja ya watuhumiwa wa tukio hilo la mauaji anatoka katika familia ya mmiliki wa gari hilo.
Vilevile, baadhi ya mali zilizokuwa ndani ya chumba cha duka linalomilikiwa na Thelesia Omary Nyambuleki Mwikoma ziliharibiwa katika vurugu hizo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawataka wananchi kutokujichukulia sheria mkononi, bali kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pale wanapobaini au kushuku kuwepo kwa vitendo vya uhalifu ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.
Chanzo na mazingira halisi ya tukio hili bado vinaendelea kuchunguzwa kwa kushirikiana na taasisi na mamlaka nyingine zinazohusika na uchunguzi utakapokamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu wote watakaobainika kuhusika na tukio la mauaji, vurugu na uharibifu wa mali.
