Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemuagiza Waziri wa Kilimo kukutana na wadau wa zao la pamba na ndani ya mwezi mmoja kuwasilisha mapendekezo ya mfumo bora wa ununuzi wa pamba utakaowanufaisha wakulima na kuendeleza uzalishaji wa zao hilo.
Ametoa agizo hilo leo, Jumatatu Septemba 14, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Itilima, mkoani Simiyu, baada ya Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Daudi Silanga, kueleza changamoto zinazowakabili wakulima wa pamba, ikiwemo malalamiko kuhusu mfumo wa sasa wa ununuzi.
“Leo tarehe 14, mpaka tunapofika tarehe 14 mwezi ujao, niwe nimeshapata taarifa ya utaratibu mzuri ambao tutakubaliana,” amesema Dkt. Mwigulu.
Amesema Serikali italinganisha mifumo iliyowahi kutumika na unaotumika sasa ili kupata utaratibu utakaokuwa na manufaa zaidi kwa wakulima bila kuathiri uzalishaji, bei ya pamba na maisha ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imeondoa sheria iliyokuwa ikiruhusu mifugo ya wananchi kutaifishwa na kuelekeza mapitio ya sheria na kanuni nyingine zinazohusiana na mifugo. Pia ameelekeza kulipwa kwa wananchi ambao mifugo yao ilitaifishwa na baadaye wakashinda kesi mahakamani.
Waziri Mkuu pia amesisitiza kuwa vyombo vya Serikali havipaswi kuchukua bodaboda, bajaji, baiskeli, mikokoteni au mali nyingine zinazotumiwa na wananchi kujipatia kipato kwa ajili ya kukusanya faini, bali faini zitolewe kwa mujibu wa sheria bila kumnyang’anya mwananchi chombo chake cha kazi.
Kuhusu bei ya saruji, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imeanza kuchukua hatua baada ya kubaini bei kufikia hadi Sh27,000, Sh30,000 na Sh32,000 katika baadhi ya maeneo, huku wataalamu wakipewa wiki moja kuandaa mpango wa kimkakati wa kurekebisha hali hiyo.
Aidha, amesisitiza kuwa mgonjwa anayehitaji rufaa hapaswi kuombwa fedha ya mafuta ya gari la wagonjwa.
“Kuanzia sasa mgonjwa asiombwe fedha ya kujaza mafuta kwenye gari la wagonjwa. Mkishamwandikia anahitaji rufaa, mtimizeni, mkimbizeni haraka,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesema Serikali imeelekeza zaidi ya Sh1.4 trilioni katika Mkoa wa Simiyu katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, katika utekelezaji wa miradi ya umeme, barabara, maji, elimu na afya.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi kutokana na mwingiliano kati ya shughuli za wananchi na wanyamapori, ikiwemo wananchi walioathiriwa na wanyamapori na wanaostahili kulipwa fidia.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Dkt. Festo John Dugange, amesema Serikali inatambua upungufu wa watumishi wa afya na elimu katika Wilaya ya Itilima. Amesema katika siku 100 za mwanzo za Serikali ya Awamu ya Sita, Itilima imepata watumishi 51 wa afya na walimu 135, huku wilaya hiyo ikipewa kipaumbele katika vibali vya ajira vitakavyotolewa kwa watumishi wa afya, elimu na kada nyingine.
Kwa upande wake, Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Daudi Silanga, amesema wilaya hiyo imeendelea kupata uwekezaji katika sekta za elimu, afya, maji, barabara na umeme, huku akiwasilisha changamoto zinazoendelea kuhitaji hatua za Serikali.

