Na Happy Lazaro, Arusha.

Wazazi na wadau wa elimu wametakiwa kuendelea kushirikiana na shule pamoja na kuongeza mchango wao katika kuboresha mazingira ya elimu, hususan kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi na mahitaji ya shule.

Rai hiyo imetolewa jijini Arusha na Mkurugenzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza Davis Preparatory, David Inzofu, wakati akizungumza katika mahafali ya 17 ya darasa la saba ya shule hiyo, ambapo jumla ya wanafunzi 77 wamehitimu.

Inzofu amesema ushirikiano wa wazazi na wadau ni muhimu katika kuhakikisha mahitaji ya shule yanaendelea kukidhiwa, akiwataka kuendelea kuiunga mkono shule na ikiwezekana kuongeza zaidi mchango wao.

Ameongeza kuwa anatarajia wahitimu hao wataendelea na elimu ya sekondari na kwamba matokeo yatakapotangazwa Januari 2027, kila mwanafunzi atakuwa amefanikiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza. Pia amewataka kutumia msingi walioupata shuleni hapo kufanya vizuri katika masomo na kudumisha nidhamu.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkuu wa wilaya ya Hai mstaafu ,Novatus Makunga, amewataka wahitimu kuzingatia maadili, nidhamu na heshima kwa wazazi na walimu, akisisitiza kuwa elimu bila maadili haina maana.

Pia amewataka kuwa mabalozi wazuri wa shule yao na kuepuka vitendo vya wizi, ulevi, vurugu, uharibifu wa mali pamoja na mahusiano na ngono za mapema zinazoweza kuvuruga ndoto na mustakabali wao.

Makunga amewahimiza kutumia teknolojia na mitandao ya kijamii kama TikTok, YouTube na akili bandia (AI) kwa hekima, hasa katika kujifunza, huku akionya dhidi ya matumizi yanayoweza kuwafanya waache kufikiri na kujifunza kwa uwezo wao wenyewe.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu, Tunu Erick amesema Davis Preparatory imeendelea kutoa elimu bora kwa kuzingatia miongozo ya elimu na kuwa na walimu wenye weledi na kujituma, jambo lililochangia mafanikio ya kitaaluma ya shule hiyo kwa miaka kadhaa.

Amesema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE), ikifanikiwa kupata ufaulu wa asilimia 100 kwa miaka kadhaa, huku ikishika nafasi za juu katika Kata ya Ambureni na Mkoa wa Arusha.

Amesema wanafunzi wameendelea kupata Daraja A, hali ambayo imeifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule zilizofanya vizuri kitaaluma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo ,Jackson Muro, amewataka wahitimu kulinda hekima, heshima, nidhamu na malezi waliyopata shuleni, wakitambua kuwa wanapoingia sekondari watakutana na walimu wapya, marafiki tofauti na changamoto mbalimbali zinazohitaji kufanya maamuzi sahihi.

Muro amesema wazazi wametumia fedha na juhudi kubwa kuwawezesha kupata elimu, huku walimu wakitumia miaka kadhaa kuwajenga kitaaluma na kitabia.

Amewataka wahitimu kujilinda dhidi ya ushawishi mbaya, akisisitiza kuwa elimu na vyeti vizuri pekee havitoshi kumhakikishia mtu mafanikio bila kuwa na hekima, heshima, adabu na tabia njema.