Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando (kushoto) akimkabidhi zawadi ya ukumbusho Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Breweries Limited (TBL) Bi. Michelle Kilpin (kulia) mara baada ya hafla ya kusainiwa kwa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya kampuni hizo mbili, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 11, 2026. Kupitia ushirikiano huo, zaidi ya wafanyabiashara 26,000 wa TBL nchini watanufaika na mafunzo ya biashara pamoja na suluhisho za kidijitali za Vodacom kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (Retailer Development Programme).

…………….

-Ushirikiano huu wa kimkakati utawawezesha wafanyabiashara wa TBL kupata suluhisho za kidijitali za Vodacom unatarajiwa kuzinduliwa rasmi jijini Mwanza Septemba 16.

Dar es Salaam, Septemba 11, 2026: Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na Vodacom Tanzania PLC leo zimeingia makubaliano ya ushirikiano (MoU) ya muda wa miaka miwili, yenye lengo la kuimarisha uwezo wa wafanyabiashara nchini kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (Retailer Development Programme), uliobuniwa mahususi ili kuwapatia ujuzi wa vitendo katika usimamizi wa biashara, fedha na matumizi ya teknolojia vitakavyopelekea kukuza biashara zao.

Ukiendeshwa chini ya kaulimbiu ya ‘Growing Innovatively Together’ (GRIT), mpango huu unadhihirisha azma ya pamoja ya taasisi zote mbili za kuwasaidia wafanyabiashara wanaoshiriki kwa kiwango kikubwa katika mnyororo wa thamani wa TBL pamoja na mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisheria na Uhusiano wa Kampuni wa TBL Neema Temba, alisema ushirikiano huu unaonesha umuhimu wa kushirikiana katika kuimarisha uwezo wa wafanyabiashara na kuwawezesha kukua kwa muda mrefu.

“Kwa TBL, wafanyabiashara ni nguzo muhimu ya biashara na ukuaji wa uchumi. Kupitia ushirikiano na Vodacom Tanzania, tunawekeza katika ujuzi, teknolojia na uendelevu wa biashara ili kuwawezesha kukuza shughuli zao na kunufaika na fursa mpya. Hivyo tunajenga thamani inayonufaisha biashara, familia na jamii kote nchini,” alisema Bi Temba.

Ushirikiano huu utaunganisha mtandao mkubwa wa TBL wa zaidi ya wafanyabiashara 26,000 na uzoefu wa Vodacom katika mawasiliano, ubunifu wa kidijitali na huduma za kifedha kimtandao, kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara kuboresha ufanisi, uimara na uendelevu wa biashara zao.

Kupitia mpango huo, wafanyabiashara watapatiwa mafunzo katika maeneo mbalimbali muhimu ya uendeshaji wa biashara, ikiwemo usimamizi wa biashara na fedha, mtiririko wa fedha, usimamizi wa bidhaa, mauzo na masoko, huduma kwa wateja, ujasiriamali, biashara inayozingatia uwajibikaji pamoja na matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Mbali na mafunzo, washiriki watawezeshwa kupata uelewa na matumizi ya suluhisho za kidijitali na kifedha zinazoweza kuwasaidia kuongeza ufanisi wa biashara, kuboresha faida na kuimarisha mahusiano na wateja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya dhamira ya Vodacom ya kutumia teknolojia na ubunifu kusaidia wafanyabiashara na kuchochea ukuaji wa biashara nchini. 

“Biashara ndogo ni muhimili wa uchumi wa Tanzania. Kupitia ushirikiano wa TBL na Vodacom Tanzania, wafanyabiashara wanapatiwa zana, maarifa na teknolojia za kuboresha biashara, kuongeza tija na kufungua fursa za ukuaji endelevu. Kwa pamoja, tunachochea ujumuishaji wa kidijitali na kifedha, na kuwawezesha kustawi katika uchumi unaoongozwa na teknolojia,” alisema Bw Nguvu.

Katika utekelezaji wa mpango huo, Vodacom itawapatia wafanyabiashara fursa ya kufahamu na kutumia suluhisho mbalimbali za biashara na huduma za kidijitali, ikiwemo SME Bomba, M-Wekeza, Lipa kwa M-Pesa na M-Koba, zinazolenga kusaidia ujumuishaji wa huduma za kifedha, ufanisi wa biashara na matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku.

Kadhalika, ushirikiano huu utakuza ubunifu, ujasiriamali na uwajibikaji katika biashara kupitia mafunzo ya ana kwa ana na majukwaa ya kidijitali. TBL na Vodacom Tanzania pia zitashirikiana katika mawasiliano, ushirikishwaji wa wadau, ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha matokeo yanayopimika na yenye manufaa ya muda mrefu. 

Mafunzo ya kwanza chini ya Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja yatafanyika Mwanza Septemba 16, yakiwapa wafanyabiashara ujuzi wa usimamizi wa biashara, fedha na matumizi ya teknolojia kwa ajili ya kuboresha utendaji na ukuaji endelevu. 

Kupitia ushirikiano huu, TBL na Vodacom zinaendelea kuimarisha ujasiriamali, matumizi ya huduma za kidijitali na kuwawezesha wafanyabiashara kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.