📍GEITA
Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi imeupitia na kuujadili Mpango wa Ufungaji wa Mgodi uliohuishwa wa AngloGold Ashanti Geita Gold Mine (GGM), ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha mpango huo unakidhi matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, pamoja na kanuni zinazohusu usalama, afya, mazingira na ufungaji wa migodi nchini.
Kikao hicho kilichofanyika katika Mgodi wa GGM, Wilaya na Mkoa wa Geita, kiliwakutanisha wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Madini, Tume ya Mipango ya Matumizi Endelevu ya Ardhi, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Tume ya Madini pamoja na viongozi wa Wilaya ya Geita.
Akiongoza kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema migodi mikubwa na ya kati inawajibika kisheria kuandaa na kuwasilisha mipango ya ufungaji migodi kwa ajili ya kufanyiwa mapitio ya kitaalamu, kujadiliwa na hatimaye kuthibitishwa endapo itakidhi vigezo vilivyowekwa.
Mhandisi Kamando amesema kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123, pamoja na Kanuni ya 206 ya Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za Mwaka 2010, wamiliki wa migodi wanapaswa kuandaa Mpango wa Ufungaji Mgodi na kuuwasilisha kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi kwa ajili ya mapitio ya kitaalamu kabla ya kuidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi.
Amesema jukumu la Kamati hiyo ni kupitia, kujadili na kuthibitisha mipango ya ufungaji migodi ili kuhakikisha shughuli za ufungaji zinazingatia matakwa ya sheria, zinalenga kurejesha mazingira katika hali inayokaribiana na hali iliyokuwepo kabla ya shughuli za uchimbaji madini na kuhakikisha ustawi wa jamii zinazozunguka migodi unaendelea hata baada ya mgodi kufungwa.
“Lengo si kufunga mgodi pekee, bali kuhakikisha mazingira yanarejeshwa na jamii inayozunguka mgodi inaendelea kuwa na fursa za kiuchumi na kijamii baada ya shughuli za uchimbaji kukoma,” amesema Mhandisi Kamando.
Kwa upande wake, Meneja wa Mazingira wa GGM, Yusuph Mhando, ameihakikishia Kamati kuwa mgodi huo umeandaa mpango wake kwa kuzingatia masuala ya usalama, afya, utunzaji wa mazingira na ustawi wa jamii inayozunguka mgodi.
Mhando amesema uongozi wa GGM utazingatia maelekezo na mapendekezo yote yatakayotolewa na Kamati hiyo na utaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika katika mchakato wa kupitia na kuboresha Mpango wa Ufungaji wa Mgodi.

