*Waziri Mavunde na Waziri Dkt. Dachun waongoza majadiliano ya ushirikiano

TIANJIN, CHINA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China zakubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya madini ili kuinua uchumi wa wananchi wa mataifa yote.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 11 Septemba, 2026 na Waziri wa Madini, *Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb)* alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Maliasili wa China, Mheshimiwa Dkt. Xu Dachun katika ukumbi wa mikutano wa Serikali Jijini Tianjin, China.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mavunde alibainisha kuwa Serikali ya China kupitia Taasisi ya Jiolojia ya China imekubali kujenga uwezo wa wataalam wa Tanzania kijiolojia na namna ya kutafsiri kwa usahihi taarifa za utafiti wa madini.

“Dhamira ya Rais wetu *Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan* ni kuona sekta ya madini inakua na kuongeza mchango wake kwenye uchumi wa nchi yetu. Ndiyo maana, Mhe. Rais ameipa sekta ya madini kipaumbele cha juu hususan katika utafiti wa kijiolojia ili kuongeza tija ya uchimbaji na manufaa kwa wananchi wa Taifa letu na uchumi kwa ujumla”

Aidha, Mhe. Mavunde alieleza kuwa China kupitia fedha za msaada (Grants) ipo mbioni kushirikiana na Tanzania katika kufanya utafiti wa kina wa madini wa kurusha ndege (High resolution airborne geophisical survey) katika bloku ya Kati inayojumuisha Mikoa ya Dodoma, Tabora, Singida na Shinyanga.

Pamoja na masuala mengine, mazungumzo hayo pia yalijikita kwenye majadiliano ya namna ya kubadilishana uzoefu na utaalam katika matumizi ya teknolojia kwenye uendelezaji wa shughuli za madini ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa mfumo wa utolewaji wa leseni.

Kwa upande wake, *Dkt. Xu Dachun* Naibu Waziri wa Maliasili wa China ambaye pia ndiye Rais wa Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia ya China (CGS) alishukuru kwa Tanzania kushiriki mkutano wa Madini China na kusisitiza kwamba yupo tayari kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuendeleza sekta zetu za madini.

Pia, Dkt. Dachun alisisitiza kuwa ushirikiano baina ya Tanzania ni China una maana kubwa na manufaa kwa pande zote mbili za Nchi kwani Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji wakati China ina teknolojia na mitaji, hivyo ushirikiano wa Nchi hizi ni wazi utaleta manufaa yenye tija kwa wananchi wa Nchi zote mbili.