NA DENIS MLOWE, IRINGA

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Bashiru Ally Kakulwa, amesema utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha ushirikiano baina ya sekta zinazogusa maisha ya wananchi ni muhimu katika kuongeza tija na kutatua changamoto za uzalishaji nchini.

Kakulwa aliyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi katika eneo la Pawaga, Wilaya ya Iringa Vijijini, Jimbo la Isimani, ambako aliungana na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, viongozi wa Serikali za Mkoa na Wilaya pamoja na wananchi kuzungumzia namna ya kuimarisha uzalishaji wa kilimo na mifugo.

Alisema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia kuhusu umuhimu wa wizara na taasisi zinazohusiana katika utendaji kazi kushirikiana badala ya kufanya kazi kwa kutenganisha sekta ambazo kwa uhalisia zinategemeana.

Kakulwa alisema kilimo na mifugo ni sekta zinazohusiana kwa karibu, hivyo ni muhimu Serikali kuweka nguvu pamoja katika kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na wafugaji, ikiwemo upatikanaji wa malisho na maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ukame unaoendelea katika baadhi ya maeneo.

“Tumekuja hapa kuungana kwa pamoja kutangaza ushirikiano katika sekta ya kilimo na mifugo kwani mahitaji katika sekta ya kilimo ni makubwa sana kwa sababu kilimo ni msingi wa usalama wa chakula na lishe ya wananchi,” alisema Kakulwa.

Aidha, alisema utekelezaji wa mpango huo unahitaji ushirikiano wa wizara mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Maji pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na mipango na upatikanaji wa rasilimali.

Alisema kila wizara ina nafasi yake katika kutatua changamoto za wananchi, akitolea mfano Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo inaweza kusaidia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo ili bidhaa zinazozalishwa ziweze kuuzwa ndani na nje ya nchi.

Kakulwa alisema Serikali pia inahitaji kuhakikisha wafugaji wanapata vipimo sahihi na vinavyotambuliwa kisheria katika biashara ya mifugo, huku mamlaka za Serikali za mitaa zikitakiwa kushirikiana na wananchi katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alisema kilimo na mifugo haviwezi kutenganishwa kwa kuwa sekta hizo mbili zinategemeana katika uzalishaji na uchumi wa wananchi.

Chongolo alisema Serikali imeamua kuanza utekelezaji wa ushirikiano huo kwa vitendo katika maeneo ambayo changamoto zake zinahitaji wizara zaidi ya moja ili kupata majawabu yenye tija kwa wananchi.

“Tukakubaliana sisi tufanye uzinduzi wa shughuli hii ya msingi ya kufanya kwa pamoja ili kuyatafuta matokeo yenye tija kwa wananchi, tukianzia hapa Pawaga, Jimbo la Isimani, Wilaya ya Iringa Vijijini,” alisema Chongolo.

Alisema baada ya kufika eneo hilo, viongozi hao wameona hali halisi ya wananchi na wafugaji, jambo ambalo limewapa nafasi ya kutambua kwa pamoja changamoto zilizopo na namna ya kuanza kuzitatua.

Chongolo pia alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James kwa kazi anayofanya katika kuhamasisha maendeleo na ubunifu wa kutatua changamoto za wananchi, akisema ushirikiano baina ya viongozi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa kwa ufanisi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ismani, Emanuela Mtatifikolo Kaganda, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika jimbo hilo, hususan mradi wa umwagiliaji ambao amesema umeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi.

Alisema pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mkoa na Wilaya katika kutatua changamoto za wafugaji, bado kuna haja ya wananchi kushiriki moja kwa moja katika kutafuta suluhisho la matatizo yanayowakabili.

Alisema baada ya kupokea malalamiko kuhusu ukosefu wa maji kwa mifugo, alifika eneo hilo wiki iliyopita kujionea hali halisi na kubaini kuwa tayari Serikali ya Mkoa na Wilaya ilikuwa imeanza kuchukua hatua.

Mtatifikolo alisema katika eneo hilo tayari kisima kimoja kilikuwa kimechimbwa kwa gharama ya Sh milioni 18, lakini changamoto iliyobaki ilikuwa upatikanaji wa pampu na mfumo wa kusukuma maji kwenda katika maeneo yanayohitaji.

Alisema kutokana na kutokuwepo kwa umeme wa uhakika katika eneo hilo, waliona ni vyema kutumia mfumo wa sola ambao ungewezesha maji kusukumwa bila kusubiri kuunganishwa kwa umeme wa kawaida.

Alisema kuwa gharama ya kufunga mfumo wa sola pamoja na pampu inakadiriwa kufikia Sh milioni tisa, ambapo yeye tayari amechangia Sh500,000 na Diwani wa eneo hilo amechangia Sh200,000, huku akiwataka wananchi na wafugaji kuendelea kuchangia ili kukamilisha mradi huo.

“Tukasema tuanze sisi kama wananchi kushirikiana tumeweka lengo ndani ya wiki mbili tuwe tumepata fedha hizo ili tuweze kutoa maji pale chini na mifugo yote ipate maji,” alisema

Alisema wafugaji wamekubaliana kuchangia fedha kwa kila boma, huku akieleza kuwa endapo kila mfugaji atachangia kati ya Sh100,000 na Sh200,000, wanaweza kufanikisha upatikanaji wa maji wakati Serikali ikiendelea kupanga namna ya kutatua changamoto nyingine.

Aliongeza kuwa wananchi wa eneo hilo wako tayari kushirikiana na Serikali na tayari wameonesha nia ya kuchangia katika kutatua changamoto za msingi.

Alisema bado kuna mahitaji ya visima vingine takribani 10 katika maeneo mbalimbali, hivyo amewataka viongozi wa Serikali na wadau wengine kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha changamoto ya maji kwa wafugaji inatatuliwa kwa awamu.

“Tunaomba viongozi watushike mkono kwenye visima vingine. Sisi tutaendelea na zoezi hili la kuhakikisha hapa tunapata maji, halafu Serikali na wadau wengine watatusaidia kule kwingine,” alisema.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya kuanza kwa utekelezaji wa mfumo wa ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kutatua changamoto za wananchi, hususan katika maeneo ambayo kilimo, mifugo, maji, viwanda na biashara vinategemeana kwa karibu.