
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini kwa kuendesha mafunzo maalum ya wiki moja yaliyolenga kujenga uwezo wa waendelezaji wa miradi midogo ya uzalishaji wa umeme unaotokana na maporomoko ya maji (Small Hydropower).
Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 7 Septemba, 2026 katika Hoteli ya Sunset mkoani Iringa, yamewakutanisha waendelezaji wa miradi (Developers) zaidi ya 15, hususan kutoka maeneo ya Nyanda za Juu Kusini. Lengo kuu ni kuwajengea uwezo wa kiufundi ili kuongeza ubora wa miradi yao ili iweze kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, tarehe 9 Septemba, 2026, Kaimu Meneja wa Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya, alisema kuwa REA haishii tu kutoa msaada wa upatikanaji wa nishati vijijini, bali inajikita pia katika kuongeza ujuzi wa wataalamu wa ndani.
“Kuongeza ujuzi kwa waendelezaji hawa kutasaidia kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na ubora unaohitajika. Hatua hii itaongeza idadi ya miradi inayofikia vigezo vya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, kuongeza uzalishaji wa umeme, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini,” alisema Mhandisi Yesaya.
Mafunzo hayo yameendeshwa kwa ushirikiano kati ya REA na Wataalamu kutoka Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia (CoET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Maeneo yaliyofundishwa ni pamoja na usanifu wa miradi, upembuzi yakinifu, sayansi ya maji (hydrology), uhandisi wa umeme na elektroniki, pamoja na uendeshaji na matengenezo ya mitambo.
Mbali na mafunzo, REA imebainisha kuwa imekuwa ikisaidia waendelezaji hao kupitia ruzuku za ujenzi, maandalizi ya maandiko ya miradi na usanifu.
Aidha, Wakala huo upo katika mchakato wa kuandaa mfumo wa mikataba ya muda mrefu (Framework Contract) na taasisi za elimu ili kutoa mafunzo endelevu kwenye nishati jadidifu ikiwemo nishati ya jua na mifumo ya gesi vunde.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wamepongeza mafunzo hayo; akizungumza na Wanahabari, Mhandisi Denis Makoyi kutoka kampuni ya Africa Power Investment, alisema mafunzo hayo yameongeza uelewa mkubwa wa kiufundi katika hatua za utekelezaji wa miradi. Naye Lutengano Kigola kutoka mradi wa Nyalawa Hydropower, aliongeza kuwa mafunzo hayo yanathibitisha kuwa Tanzania ina wataalamu wa ndani wenye uwezo mkubwa wa kuendeleza miradi ya umeme wa maji.
