…………………………………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
MCHEZAJI mkongwe aliyewahi kucheza katika vilabu mbalimbali nchini ikiwemo timu ya Taifa (Taifa Starts) Douglas Mhani, amewataka wachezaji kufanya mazoezi binafsi ili kujiweka fiti.
Mhani alitoa rai hiyo mkoani hapa,ambapo alisema tangu ugonjwa wa corona uingie nchini, hatua mbalimbali zinachukuliwa na serikali kuhakikisha tunapambana nao, huku madaktari bingwa ulimwenguni wakiendelea kutafuta tiba.
“Tangu kuibuka kwa ugonjwa huo wa Corona hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na serikali yetu, ambapo kupitia Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alitangaza kusimamishwa kwa michezo na shule mbalimbali, hatua hiyo haimzuii mchezaji kufanya mazoezi ya peke yake,” alisema Mhani.
Alisema kuwa kwa kipindi hiki ambacho michezo imesitishwa kupisha ugonjwa huo, kwa wachezaji wanatakiwa kujifua binafsi ili kutoshuka viwango vyao, kwani ligi itakapoanza tena makocha hawatokuwa tayari kuwatumia wachezaji watakaowaona viwango vyao vimeshuka ama kukosekana kwa pumzi.
“Serikali kupitia Waziri Mkuu alipotangaza kusitishwa kwa michezo, mikusanyiko pamoja na kufunga shule na vyuo, haikuwakataza wanamichezo kufanya mazoezi binafsi, hivyo wachezaji waendelee na mazoezi ili Ligi itakapoanza wawe vizuri,” alisema Mhani.
Akizungumzia kusitishwa au kufutwa kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mchezaji huyo aliyekuwa kiungo mwenye nguvu awapo uwanjani alisema hali hii ikifika mpaka mwezi wa sita, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF huenda wakalazimika kufanya hivyo.
“Ligi zote duniani zinaanzia mwezi wa sita -saba kwa kila mwaka, na kumalizika mwezi mei mwaka unaofuatia kwa mfano 2019/2020 inayotarajia kufikia tamati mwezi mei, tunamuomba Mwenyezimungu janga hili liishe haraka, lakini kinyume chake hali itakuwa hivyo,” alisema Mhani.