Na.Sophia Kingimali

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam imeunga mkono maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa yaliyofanyika Agosti 26, 2026, ikiwemo uamuzi wa kumvua uanachama wa chama hicho Ndg. Emmanuel John Nchimbi.

Akisoma Tamko hilo leo Septemba 7,2023 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu, baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa kilichofanyika Septemba 6, 2026 katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine kilijadili masuala mbalimbali yanayohusu chama na Taifa.

Amesema Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa imepongeza uamuzi uliofanywa na CCM Taifa dhidi ya Nchimbi, ikieleza kuwa hatua hiyo imezingatia maslahi mapana ya Taifa pamoja na masharti yaliyoainishwa katika Ibara ya 103(8) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 na Ibara ya 50(2)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Aidha, Halmashauri Kuu hiyo imempongeza Deogratius Ndenjembi kwa kupendekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuthibitishwa na Bunge na hatimaye kuapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

CCM Mkoa wa Dar es Salaam imesema Ndenjembi anastahili pongezi kwa kuaminiwa kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa Taifa, huku ikimtaka kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kwa kuzingatia dhamana aliyopewa katika kuwatumikia Watanzania.

Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam imeeleza kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi anayoifanya katika kukijenga chama pamoja na kuendeleza maendeleo ya nchi.

Mtemvu amesema chama hicho kinamtakia Rais Samia afya njema na kazi njema katika utekelezaji wa majukumu yake, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi na wanachama kuendelea kushirikiana katika kuimarisha CCM na kuchangia maendeleo ya Tanzania.