Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Serikali imesema sayansi, teknolojia na ubunifu ni nyenzo muhimu katika kuongeza mchango wa uchumi wa bluu nchini, ikisisitiza umuhimu wa tafiti na matumizi ya teknolojia katika kuibua fursa zilizopo kwenye bahari, maziwa, mito na maeneo ya pwani.
Pia,imeitaka sekta binafsi kuchangamkia fursa za uchumi wa bluu, ikiwemo teknolojia za baharini, kuongeza thamani ya mazao ya bahari na huduma za kidijitali, ili Tanzania iweze kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 7,2026 Jijini Dar es salaam wakati wa kufunguliwa kwa Kongamano la Tano la Kimataifa la Sayansi na Uchumi wa Bluu lililowakutanisha wataalamu, watafiti, watunga sera na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Deogratius Ndejembi, ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi lakini alishindwa kuhudhuria kutokana na msiba uliotokea katika familia ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais muungano na mazingira Mhandisi Hamadi Masauni alisema Tanzania ina rasilimali nyingi za majini ambazo zina uwezo mkubwa wa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Alisema uchumi wa bluu si dhana mpya kwa Tanzania kwa kuwa rasilimali za bahari, maziwa, mito, maeneo oevu na mifugo ya majini zimekuwa sehemu ya maisha ya Watanzania kwa muda mrefu, huku akisisitiza kuwa rasilimali hizo zinapaswa kutumika kwa tija bila kuathiri mazingira Kwani, sekta hiyo inaweza kuongeza ajira, usalama wa chakula, biashara, uwekezaji na mapato ya Taifa.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira ya kisera na kitaasisi kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa bluu, ikiwemo kuimarisha uratibu wa masuala hayo kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar. Hatua hizo zinaenda sambamba na utekelezaji wa mipango ya muda mrefu inayolenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaotumia teknolojia na ubunifu.
Ameongeza kuwa mafanikio ya uchumi wa bluu yanategemea kwa kiasi kikubwa tafiti za kisayansi na ubunifu, hivyo watafiti wanapaswa kuendelea kufanya tafiti zitakazosaidia kufahamu ukubwa wa rasilimali zilizopo, kuongeza uzalishaji, kubuni teknolojia mpya, kuongeza thamani ya mazao ya baharini na kulinda mazingira.
Aidha,amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ili kuongeza ufanisi wa biashara na kuchochea uchumi wa bluu ambapo Miongoni mwa hatua hizo ni maboresho ya reli ikiwemo SGR, pamoja na kuimarisha miundombinu ya bandari ili kupunguza gharama na muda wa usafirishaji na kuongeza ushindani wa Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika eneo la usafiri wa majini, Serikali inaendelea na ukarabati wa meli zilizopo katika maziwa mbalimbali nchini pamoja na ujenzi wa meli mpya. Pia imeanza ujenzi wa kiwanda cha kujenga meli Katavi, huku kukiwa na mipango ya kuongeza uwezo wa kujenga na kukarabati vyombo vya majini kwa ajili ya usafirishaji, uvuvi, utalii na shughuli nyingine za uchumi wa bluu.
Vilevile, Serikali imeeleza kuwa inaendelea na ujenzi na maandalizi ya vyombo vya uokoaji katika maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyika, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa usafiri wa majini. Hatua hizo zimeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kukamilisha mnyororo wa huduma za uchumi wa bluu na kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali zao.
Akihitimisha, mhasndisi Masauni amewataka wataalamu na watafiti walioshiriki kongamano hilo kuwasilisha mapendekezo yanayoweza kutekelezeka na yatakayosaidia kuboresha sera, kuongeza uwekezaji, kuimarisha ulinzi wa rasilimali za majini na kuongeza matumizi ya teknolojia.

