Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

WIZARA ya Katiba na Sheria imesema inaendelea kuhakikisha kuwa sera na sheria zinazosimamia utajiri wa asili, maliasili na uchumi wa bluu zinakuwa rafiki na wezeshi kwa uwekezaji, huku zikilinda maslahi ya Taifa na kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali hizo.

Akizungumza katika Kongamano la Kimataifa la Uchumi wa Bluu, Neema Mwanga Mkurugenzi kitengo cha uangalizi wa usafiri asilia na maliasili wa Wizara hiyo ameeleza kuwa uchumi wa bluu unahusisha shughuli mbalimbali zinazofanyika katika bahari, maziwa na maeneo mengine yenye rasilimali za maji, hivyo kunahitajika mfumo madhubuti wa kisheria unaoweza kusimamia matumizi ya rasilimali hizo kwa maendeleo endelevu.

Amesema kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kuna umuhimu wa kuweka uwiano kati ya jukumu la kuvutia uwekezaji na wajibu wa kusimamia utajiri wa asili na maliasili za nchi ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanafikiwa kwa njia endelevu.

Ameongeza kuwa sheria ambazo zinaweza kuwa kikwazo katika kuvuna, kutumia na kuwekeza katika rasilimali za asili, ikiwemo uchumi wa bluu, zinapaswa kufanyiwa marekebisho ili kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, hususan katika sekta kama uvuvi wa baharini na ufugaji wa samaki.

“Sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufanikisha malengo ya Dira 2050, hivyo mazingira ya kisheria yanapaswa kuwa wezeshi kwa wawekezaji huku yakihakikisha uwekezaji unaofanyika unazalisha manufaa ya kiuchumi kwa wananchi”,Amesema.

Katika hatua nyingine, Wakili Daniel Mbaki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria amesema Wizara hiyo ina kitengo maalumu cha utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, kinacholenga kusaidia kutatua migogoro inayoweza kujitokeza kati ya wawekezaji na wadau mbalimbali bila kutegemea zaidi taratibu za mahakama.

Amesema Wizara imesajili wataalamu wanaotoa huduma za utatuzi wa migogoro, wakiwemo wapatanishi na wasuluhishi, huku akiwataka watu wanaotaka kutoa huduma hizo kufuata taratibu za usajili kupitia mfumo wa NARIS uliowekwa na Wizara.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Richard Jacopiyo amesema mfumo imara wa kisheria ni nyenzo muhimu katika kuweka mazingira ya uwekezaji yanayozingatia maslahi ya Taifa, akisisitiza kuwa sheria zinapaswa kwenda sambamba na malengo ya Dira 2050 katika kukuza uchumi na maendeleo ya kijamii.