Mbunge wa Mbinga Vijijini na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Salvio Kapinga, akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Joseph Kashushura, wamekutana na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, Septemba 4, 2026, jijini Dodoma, kujadili changamoto zinazotokana na shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe mkoani Ruvuma.
Katika kikao hicho, viongozi hao waliwasilisha kero za wananchi kuhusu ulipaji wa fidia kwa wanaoathiriwa na shughuli za uchimbaji, utekelezaji wa Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR), pamoja na baadhi ya kampuni kutotekeleza kwa wakati wajibu mbalimbali unaohusiana na maeneo wanayofanyia shughuli.
Mhe. Kapinga amesema changamoto hizo zimekuwa zikigusa maisha ya wananchi, ikiwemo upatikanaji wa maji, barabara na huduma za afya, hivyo kuomba Wizara ya Madini kuchukua hatua kuhakikisha kampuni zinazofanya shughuli za uchimbaji zinatimiza wajibu wao kwa jamii.
Akijibu hoja hizo, Mhe. Mavunde ameahidi kuwa Wizara yake itashughulikia changamoto hizo ndani ya mwezi mmoja, huku akiiagiza Tume ya Madini kufika mkoani Ruvuma na kukutana na wamiliki wa migodi pamoja na wananchi kwa ajili ya kutafuta suluhu na kuhakikisha changamoto zinazohusiana na shughuli za uchimbaji zinapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wameshauri kuwekwa kwa mikakati madhubuti ya kukusanya madeni ya mapato yanayokaribia asilimia 70.

