Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Jumamosi, Septemba 5, 2026, amekagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na kuweka jiwe la msingi la mradi huo, unaolenga kuboresha mazingira ya utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Kaimu Mhandisi wa Wilaya ya Bahi, Sassoche Mtenya Maduhu, amesema jengo hilo linatarajiwa kugharimu jumla ya Sh bilioni 4.868 na litajengwa kwa awamu.

Amesema hadi kufikia Agosti 30, 2025, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ilikuwa imepokea jumla ya Sh bilioni 1 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo hilo, ambapo Sh milioni 994.546 zimetumika.

Katika fedha hizo, Sh milioni 980.247 zimetumika kumlipa mkandarasi M/s Hamble Ulpan Engineering Company Limited, huku Sh milioni 14.3 zikitumika kwa ununuzi wa vyuma vilivyoagizwa kutoka Kiwanda cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi umefikia asilimia 100, ukiwa umehusisha maandalizi ya eneo la ujenzi, uchimbaji na ujenzi wa msingi, ujenzi wa nguzo na ring beam, ujenzi wa kuta pamoja na uwekaji wa mifumo ya awali ya maji, umeme na TEHAMA.

Mradi huo pia umechangia ajira 152 kwa wananchi, wakiwemo wanawake 89 na wanaume 63, huku kukamilika kwake kukitarajiwa kuimarisha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi wa watumishi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bahi, Mhe. Kenneth Nollo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo, akisema litakapokamilika litakuwa jengo la kisasa litakaloboresha mazingira ya kazi na utoaji wa huduma katika Halmashauri hiyo.