Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, *Mhe. Samwel M. Maneno* amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lililopo Mtumba Jijini Dodoma, lengo likiwa ni kujionea hatua zilizofikiwa pamoja na kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa viwango vilivyokusudiwa na kwa wakati.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amefanya ziara hiyo tarehe 4 Septemba, 2026 ambapo alikagua maeneo mbalimbali ya mradi huo ikiwa ni pamoja na mifumo ya umeme na TEHAMA, eneo la maegesho ya magari vyumba vya ofisi, na kumbi za mikutano.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa, ukamilishaji wa jengo hilo utakuwa chachu kubwa katika kuboresha mazingira ya kazi kwa Mawakili na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, jambo litakaloongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kisheria kwa wananchi
Mhandisi Evance Mwingizi anayesimamia mradi huo kutoka SUMA JKT, amesema mradi huo umefikia asailimia 80, na kazi zinaendelea kulingana na mpango kazi uliowekwa.
Aidha, Mhandisi Mwingizi ameeleza kuwa kazi zinazoendelea ni pamoja na ukamilishaji wa kazi za kupaka rangi, kuweka vioo, kuweka milango, mifumo ya Umeme na TEHAMA na eneo la maegesho ya magari.
