NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, ameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro wa fidia ya wananchi 23 waliopisha ujenzi wa barabara ya Iringa–Dodoma, ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 22 bila wananchi hao kulipwa stahiki zao.
Akizungumza Bungeni wakati akiuliza swali la nyongeza, Ngajilo alisema wananchi hao waliondolewa katika maeneo yao wakati wa upanuzi wa barabara hiyo mwaka 2004, ambapo jumla ya wananchi 38 walihusika, lakini ni 15 pekee waliolipwa fidia huku 23 wakibaki bila malipo hadi sasa.
Alisema hali hiyo imeendelea kuwa kero kubwa kwa wananchi wa Kihesa Kilolo na imekuwa ikiwafanya kulalamika mara kwa mara, jambo ambalo kwa mujibu wa mbunge huyo linaweza pia kuathiri hali ya kisiasa katika eneo hilo.
“Wananchi 15 tu walilipwa, wananchi 23 hawakulipwa. Hii imekuwa kero mpaka leo wanailalamikia. Serikali ya mtaa inawatambua, Serikali ya kata inawatambua na hata mabaraza yanawatambua, imekuwaje TANROADS haiwatambui wananchi hawa 23?” alihoji Ngajilo.
Mbunge huyo alitaka kujua iwapo Waziri yuko tayari kushughulikia mgogoro huo wa muda mrefu ili wananchi hao waweze kupata haki zao na kuishi kwa amani.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi Godfrey Kasekenya alieleza kuwa suala hilo linahusu fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya Iringa–Dodoma na kwamba ni muhimu kufanyika kwa tafsiri ya sheria iliyokuwepo wakati wananchi hao waliondolewa pamoja na sheria inayotumika sasa.
Alisema inawezekana wananchi hao waliondolewa katika maeneo yao, lakini huenda baadhi yao hawakuwa ndani ya eneo lililotambuliwa kisheria kuwa linastahili fidia wakati huo.
“Pengine waliondolewa lakini walikuwa ndani ya fidia, na kama hivyo ndivyo ilivyo kwa sheria yetu, hawawezi kupata fidia. Lakini kama barabara iliwafuata au walikuwa nje ya zile mita 45 kwa wakati huo, basi tunapaswa kuwalipa,” alisema Waziri.
Waziri Kasekenya aliahidi kushirikiana na Mbunge Ngajilo pamoja na wataalamu wa TANROADS ili kufuatilia suala hilo na kubaini sababu za wananchi hao kutolipwa, ikiwa watathibitika kuwa walikuwa na haki ya kulipwa fidia.
Alimwomba Mbunge Ngajilo kukutana naye pamoja na uongozi wa TANROADS kwa ajili ya kupitia kwa kina nyaraka na mazingira ya wananchi hao 23, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
“Ni suala la miaka 22, baada ya hapa tuweze kuonana, tukutane na wenzetu wa TANROADS kuona kwanini hawa watu, kama wana haki, wasipate haki yao,” alisema Waziri.
