Na Mwandishi wa OTR
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) imeendelea na hatua za kuimarisha mifumo yake ya utendaji kwa kuwajengea uwezo watumishi kuhusu Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (Quality Management System – QMS), unaolenga kuiwezesha taasisi kufikia viwango vya kimataifa vya ubora.
Mafunzo hayo yaliyotolewa Ijumaa, Septemba 4, 2026 jijini Dar es Salaam na kampuni ya Amaxon, ni sehemu ya maandalizi ya OTR kuelekea kupata ithibati ya ubora kimataifa (ISO 9001:2015), ambayo inaweka viwango vya kimataifa vya usimamizi wa ubora katika taasisi na mashirika.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji wa Taasisi za Kibiashara alisema utekelezaji wa QMS utasaidia OTR kuimarisha mifumo ya kazi, kuongeza ufanisi na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia mahitaji ya wadau.
“Tunataka kutambulika kimataifa kama taasisi inayofuata viwango vya ubora wa kimataifa katika utoaji wa huduma,” alisema Bi. Mauki.
Alisema kufikia kiwango hicho kunahitaji ushiriki wa watumishi wote na utekelezaji wa taratibu zinazoweka wazi namna kazi zinavyopaswa kufanyika, kufuatiliwa na kutathminiwa.
Mafunzo kwa watumishi hao yalitanguliwa na programu ya wiki moja ya kuwajengea uwezo QMS Champions kutoka kila idara na kitengo cha OTR, iliyowapa ujuzi kuhusu matumizi ya misingi ya usimamizi wa ubora katika shughuli za kila siku, pamoja na namna ya kufanya ukaguzi wa ndani wa mifumo ya kazi.
QMS Champions hao wanatarajiwa kuwa na nafasi muhimu katika kuhamasisha na kusaidia utekelezaji wa QMS katika maeneo mbalimbali ya kazi, ili kuhakikisha mfumo huo unaeleweka na unatekelezwa ipasavyo katika shughuli za taasisi.

