…………..
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kushirikiana na wananchi pamoja na wadau wengine katika kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha na mali za wananchi, kwa kuendeleza mikakati ya kubaini na kuzuia uhalifu.

Mnamo Agosti 29, 2026, saa 5:45 usiku, huko Shewa, Kata ya Mwakibete, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya, Vaileth Libaba (34), aliyekuwa mfanyabiashara wa miamala ya fedha, alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya baada ya kuvamiwa na watu watano.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu hao walimchoma kwa kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili na kumpora fedha taslimu Shilingi 300,000 pamoja na simu mbili za mkononi zilizokuwa zikitumika katika biashara yake ya miamala ya fedha.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya liliendelea na ufuatiliaji wa watu waliohusika na tukio hilo.

Septemba 3, 2026, majira ya saa 5:00 usiku, Polisi walipokea taarifa kwamba baadhi ya watuhumiwa waliodaiwa kuhusika katika tukio la Agosti 29, 2026, walikuwa eneo la Ituha Relini wakivuta bangi.

Askari walifika katika eneo hilo na kuwabaini watu watatu. Hata hivyo, kabla ya kuwakamata, mmoja wa watuhumiwa, aliyetambuliwa kwa jina la Venance Yasin, alitoa bastola iliyotengenezwa kienyeji na kutaka kumpiga risasi askari aliyekuwa akimkamata.

Katika kumuokoa askari huyo, askari mwingine alifyatua risasi na kumjeruhi mtuhumiwa huyo.

Mtuhumiwa mwingine, aliyetajwa kwa jina la Atupele Kabale, ambaye alikuwa ameshika rungu, alimshambulia askari kwa kumpiga begani na kisha kuanza kukimbia.

Hali hiyo ilimfanya askari huyo kufyatua risasi tatu hewani kwa lengo la kumtahadharisha na kumtaka asimame, lakini mtuhumiwa aliendelea kukimbia. Askari alifyatua risasi iliyompata katika paja la mguu wa kulia.

Watuhumiwa hao wawili walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa ajili ya matibabu kutokana na majeraha waliyoyapata, lakini wote wawili walifariki dunia wakiwa wanaendelea kupatiwa matibabu.

Katika upekuzi, lilipatikana begi moja la mgongoni lililokuwa na kisu kimoja, panga moja, mizula miwili pamoja na silaha aina ya bastola iliyotengenezwa kienyeji, ambayo kwa mujibu wa taarifa hiyo ina uwezo wa kutumia risasi za shotgun.

Aidha, ufuatiliaji umebaini kuwa mtuhumiwa Venance Yasin, maarufu kwa jina la Mnyaki, alitoroka gerezani mwaka 2025 wakati akitumikia kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la wizi wa gari alilolitenda Oktoba 11, 2023, eneo la Forest, Mbeya.

Kwa upande wake, mtuhumiwa Atupele Kabale aliwahi kushtakiwa kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, ambapo alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela Januari 6, 2025.

Baadaye aliachiwa huru na Mahakama ya Rufaa baada ya kukata rufaa katika Mahakama hiyo Februari 13, 2026.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kuwashikilia watuhumiwa wengine watatu kwa ajili ya mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo. Watuhumiwa hao walikamatwa katika msako uliofanyika kufuatia tukio la mauaji na matukio mengine ya uhalifu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa wito kwa wananchi wanaomiliki silaha kihalali, lakini wanazitumia katika matukio ya uhalifu, kuacha mara moja matumizi hayo na kusalimisha silaha hizo kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa katika taarifa ya umma kuhusu kampeni ya usalimishaji silaha kwa hiari.

Aidha, Jeshi hilo limewataka wananchi wenye tamaa ya kujipatia fedha au mali kwa njia zisizo halali kwa kufanya uhalifu kuacha mara moja, likisisitiza kuwa uhalifu haulipi na hauna nafasi katika jamii.