Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo na viongozi wengine wa taasisi hiyo wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa mashine ya kisasa ya uchunguzi wa saratani ya matiti (Mammography) iliyonunuliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi milioni 800. Mashine hiyo yenye teknolojia ya akiliunde (Artificial Intelligence – AI) inabaini na kuonesha maeneo yenye viashiria vya tatizo katika picha za uchunguzi hatua itakayosaidia kuimarisha uchunguzi na utambuzi wa mapema wa saratani ya matiti.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu uzinduzi wa mashine ya kisasa ya uchunguzi wa saratani ya matiti (Mammography) iliyonunuliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi milioni 800. Mashine hiyo yenye teknolojia ya akiliunde (Artificial Intelligence – AI) inabaini na kuonesha maeneo yenye viashiria vya tatizo katika picha za uchunguzi hatua itakayosaidia kuimarisha uchunguzi na utambuzi wa mapema wa saratani ya matiti.

Daktari Bingwa Mbobezi wa Radiolojia wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Anganile Kalinga akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mashine ya kisasa ya uchunguzi wa saratani ya matiti (Mammography) iliyopo katika taasisi hiyo inatumia teknolojia ya akiliunde (Artificial Intelligence – AI) kubaini na kuonesha maeneo yenye viashiria vya tatizo katika picha za uchunguzi na utambuzi wa mapema wa saratani ya matiti. Picha na ORCI

………..

Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) imeongeza uwezo wake wa kutoa huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti baada ya kuzindua mashine mpya ya Mammography inayounganishwa na teknolojia ya akiliunde (Artificial Intelligence – AI) hatua inayolenga kuimarisha utambuzi wa ugonjwa huo katika hatua za awali.

Ujio wa teknolojia hiyo ni sehemu ya uwekezaji katika huduma za kisasa za saratani huku mashine hiyo ikiwa na uwezo wa kusaidia wataalamu kuchanganua picha za matiti na kuainisha maeneo yanayoweza kuwa na viashiria vya ugonjwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashine hiyo leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo alisema upatikanaji wa teknolojia hiyo umewezekana kutokana na hatua ya Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwezesha ununuzi wake.

Alisema Serikali ilitoa shilingi milioni 600 ambazo hazikuwa sehemu ya bajeti ya awali baada ya kubaini umuhimu wa mashine hiyo katika kuboresha huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti.

“Tunaishuku Serikali ya awamu wa sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa mashine hii. Gharama yake ilikuwa shilingi milioni 800 lakini tuliipata kwa shilingi milioni 600”, alisema Dkt. Msemo.

Alisema tofauti kubwa ya mashine hiyo na teknolojia iliyokuwa ikitumika awali ni uwezo wa mfumo wa AI kumsaidia mtaalamu kuangalia maeneo yanayoweza kuwa na tatizo na kuyafanyia uchambuzi kwa umakini zaidi.

Kwa mujibu wa Dkt. Msemo teknolojia hiyo pia inalenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa kupunguza muda unaotumika katika uchambuzi wa picha na kuongeza idadi ya watu wanaoweza kufanyiwa uchunguzi.

“Wagonjwa zaidi ya 20 kwa siku wanaweza kuchukuliwa sampuli na kuchunguzwa kupitia mashine hiyo, ili  kuhakikisha teknolojia hii inatumika kwa ufanisi, wataalamu wa tatu watakwenda  nchini Uturuki kwa mafunzo maalumu ya matumizi ya mashine hiyo”, alisema.

Dkt. Msemo ambaye pia ni Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Saratani na Mionzi alisema uwekezaji huo una umuhimu mkubwa kutokana na saratani ya matiti kuwa miongoni mwa saratani zinazoongoza kwa wanawake duniani na kuwa ya pili kwa wagonjwa wanaohudumiwa ORCI baada ya saratani ya mlango wa kizazi.

Alisema kati ya wagonjwa wa saratani wanaofika ORCI, kati ya asilimia 10 na 12 wanakabiliwa na saratani ya matiti  hivyo kuimarisha uwezo wa uchunguzi ni sehemu muhimu ya kupunguza athari za ugonjwa huo.

Kwa upande wake Daktari Bingwa Mbobezi wa Radiolojia na mtumiaji wa mashine hiyo Anganile Kalinga alisema mfumo wa akiliunde (AI) unaongeza uwezo wa wataalamu katika kuchambua picha za matiti na kutambua maeneo yenye viashiria vinavyoweza kuhitaji uchunguzi wa kina zaidi pamoja na kuchukuwa sampuli kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Alisema teknolojia hiyo inaweza kutumika si kwa wagonjwa wanaoonyesha dalili pekee, bali pia kwa watu ambao bado hawajabaini dalili zozote hivyo kutoa fursa ya kugundua mabadiliko ya awali yanayoweza kuashiria uwepo wa saratani ya matiti.

Dkt. Kalinga alieleza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yanaongeza ufanisi katika uchunguzi wa saratani ya matiti kwa kumsaidia mtaalamu kupata taarifa muhimu kutoka kwenye picha za uchunguzi kwa wakati hali inayoweza kurahisisha hatua zinazofuata za uchunguzi na kusaidia mgonjwa kupata huduma stahiki mapema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Impilo Technologies Limited ambao ni wasambazaji wa mashine hiyo, Onesmo Haule alisema mashine hiyo imekuja kuongeza uwezo wa wataalamu kutumia teknolojia ya kisasa katika uchunguzi wa saratani ya matiti ikiwemo kuwasaidia kupata na kuchambua taarifa muhimu kutoka kwenye picha za uchunguzi kwa ufanisi zaidi.

“Uwekezaji uliofanywa na ORCI katika kuboresha huduma za matibabu ya saratani nchini si kuongeza mashine pekee  bali ni kuongeza uwezo wa wataalamu, kupanua huduma za uchunguzi na kuwapa wananchi fursa ya kugundua saratani ya matiti mapema zaidi”,  alisema Haule.

Baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kufanyiwa uchunguzi kwa kutumia mashine hiyo wameeleza kufurahishwa na huduma hiyo na kusema kuwa imewasaidia kuokoa muda wa kusubiri kufanyiwa uchunguzi.

Sophia Kishavi mkazi wa Kitunda jijini Dar es Salaam alisema amefurahishwa na kupata huduma hiyo na kwamba uchunguzi ulikuwa wa muda mfupi.

“Nimefanyiwa uchunguzi bila malipo, kwa kawaida uchunguzi ni shilingi 80,000 lakini mimi sikuwa na fedha ya kulipia. Naishukuru Taasisi imenipa msamaha wa matibabu nimepimwa bure.

“Ni muhimu wananchi kuchukua hatua za kufanya uchunguzi wa saratani kwa wakati badala ya kusubiri dalili za ugonjwa kujitokeza”,  alisema.

Warda Bakari mkazi wa Mbagala  alisema upatikanaji wa teknolojia hiyo ni muhimu kwa wananchi hasa kwa wale wenye uwezo mdogo wa kifedha ambao wanaweza kushindwa kumudu gharama za vipimo.

“Ninaishukuru Serikali kwa kuwekeza katika vifaa tiba vya kisasa hapa ORCI, pia ninaushukuru uongozi wa taasisi hii kwa kunipa nafasi ya kufanya kipimo hiki bila gharama yoyote ile kwani sikuwa na fedha za kulipia vipimo”, alishukuru Warda.

Uzinduzi wa mashine hiyo unaweka msisitizo mpya katika matumizi ya teknolojia katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa saratani nchini. Hatua inaendana na juhudi za kuendelea kuboresha huduma za saratani kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Kuwepo kwa  mashine hiyo kutaimarisha upatikanaji huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti nchini na kuongeza uwezo wa ORCI kutoa huduma bora zenye ufanisi zaidi huku ikisaidia wataalamu kubaini viashiria vya ugonjwa kwa wakati na kuwapa wananchi fursa ya kufanya  uchunguzi na kupata matibabu mapema.