Kwa mara ya kwanza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefanikiwa kumfanyia upasuaji wa moyo mtoto wa siku mbili aliyezaliwa akiwa na tatizo la kubana kwa mshipa wa damu unaopeleka damu kwenye mapafu (Severe pulmonary valve stenosis).

Upasuaji huo wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Percutaneous balloon pulmonary valvuloplasty- PBV) umefanyika akatika kambi maalumu ya siku sita iliyokuwa ikifanywa na watalaamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa shirika la Muntada Aid lililopo nchini Uingereza.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema ushirikiano huo wa kimatibabu umeleta matokeo makubwa ikiwemo kufanikiwa kumfanyia upasuaji mtoto wa siku mbili.

“Hii ni mara yetu ya kwanza kumfanyia mtoto wa umri huu, mafanikio haya ni matokeo ya msaada wa vifaa tiba uliofanywa na shirika hili pamoja na serikali yetu ya Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi na kufanikisha upasuaji huu,” alisema Dkt. Angela.

Aidha Dkt. Angela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi alisema jumla ya Watoto 44 wamefanyiwa upasuaji mdogo na mkubwa ambapo watoto 28 wamefanyiwa upasuaji kwa njia ya tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab huku watoto 16 wakifanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua.

“Kupitia kambi hiyo wataalamu kutoka shirika la Muntada Aid wamekuja na vifaa tiba vyenye thamani ya milioni 50 ili kwa pamoja tuweze kuwasaidia watoto wengi wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo”, alisema Dkt. Angela

Katika hatua nyingine Dkt. Angela alitoa rai kwa wanawake wajawazito kufanya uchunguzi wa mapema ili kubaini changamoto za moyo kwa mtoto ili waweze kuwasaidia watoto na kuokoa maisha yao.

“Wazazi wa watoto wenye magonjwa ya moyo wengi wao utufikia wakiwa wamechelewa na matokeo ya kimatibabu yanakuwa siyo mazuri sana hivyo tunawahamasisha wafike mapema ili kupunguza changamoto hizo kwani JKCI tunatoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo mapema kuwalinda watoto”, alisema Dkt. Angela

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Muntada Aid Nayaf Sheikh alisema shirika hilo limesafiri katika mataifa mbalimbali kuwasaidia watoto wanaohitaji upasuaji wa kibingwa lakini limeona upekee wa JKCI kutokana na kuwa na miundombinu wezeshi.

“Hii ni mara yetu ya 9 kuja JKCI na mara zote ambazo tumekuwa tukija hapa tumekuwa tukipewa ushirikiano wa watalamu ambao unatuwezesha kufanya upasuaji wa kibingwa kwa kiwango kikubwa hivyo watanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla hawana haja tena ya kusafiri kwenda nje ya nchi kufuata matibabu ya kibingwa”, alisema Sheikh.