Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) Mhe. Deus Sangu akiteta jambo na Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Waithna’ashariyyah Tanzania (TIC) Sheikh Hemed Jalala (Kushoto) Pamoja na Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiyah ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Sheikh Alhad Mussa Salum (Kulia) katika hafla ya kumbukizi ya mazazi ya Mtume Muhammad (Sallallahu Alayhi Wasallam) iliyofanyika Agosti 30,2026 katika uwanja wa Kigogo Posti, Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) Mhe. Deus Sangu akiteta jambo na Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Waithna’ashariyyah Tanzania (TIC) Sheikh Hemed Jalala (Kushoto) Pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kinondoni Mhe. Abbas Tarimba (Kulia) katika hafla ya kumbukizi ya mazazi ya Mtume Muhammad (Sallallahu Alayhi Wasallam) iliyofanyika Agosti 30,2026 katika uwanja wa Kigogo Posti, Jijini Dar es Salaam.

Na: OWM (KAM), Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu ametoa wito kwa wananchi na Taasisi za dini kuendelee kushirikiana na Serikali katika kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa misingi hiyo ni nguzo muhimu katika kujenga Taifa imara. 

Aidha, pia amewasihi kuhusu suala la malezi bora na uadilifu kwa watoto na vijana ili kuepuka athari za mmomonyoko wa maadili pamoja na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto, kwa lengo la kujenga kizazi kijacho chenye maadili na upendo.  

Mhe. Sangu ametoa wito huo (Jumapili, Agosti 30, 2026) alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika hafla ya kumbukizi ya mazazi ya Mtume Muhammad (Sallallahu Alayhi Wasallam) iliyofanyika katika uwanja wa Kigogo Posti, Jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali inatambua mchango wa Taasisi za Dini katika kuimarisha mshikamano wa kijamii; kukuza maadili ya uadilifu, uwajibikaji na upendo; kutoa huduma za kijamii kama vile elimu, afya na msaada wa kijamii pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa amani na mshikamano wa kitaifa

“Serikali inatambua nafasi ya Jumuiya ya Waithna’ashariyyah Tanzania (TIC), ikiongozwa na Sheikh Mkuu wa TIC Maulana Sheikh Hemed Jalala na taasisi zote za dini katika kuimarisha mahusiano mema, amani na utuivu,” amesema

Kadhalika, ametoa wito kwa waumini wa dini ya kiislamu kuyashika na kuyaishi kwa vitendo mafundisho na Maisha ya Mtume Mohammad (S.A.W) dini hususan katika kuimarisha maadili, upendo, amani na mshikamano katika jamii ili kujenga Taifa lente maadili mema na uwajibikaji.

Kwa upande mwengine, Waziri Sangu amewasilisha salamu za Sikukuu ya Maulid kutoka kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba na pia kuwapongeza kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kudumisha Amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Pia, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Waithna’ashariyyah Tanzania (TIC) Sheikh Hemed Jalala,ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa nia njema ya kushiriki katika Sherehe za Maulid, akisema ushiriki huo ni ishara ya ushirikiano mzuri kati ya Serikali na jamii. Aidha, upendo na Huruma ndo Mafunzo ya Mtume Muhammad (S.W.W) ampapo amezitaka taasisi zote za dini kuendeleza juhudi za kuwaleta pamoja waumini na wasiokuwa waumini kupitia mihadhara na shughuli mbalimbali za kidini zinazolenga kumuenzi na kumsifia Mtume Muhammad (S.W.W), huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano na umoja katika jamii.