Na.Sophia Kingimali.Dar es salaam
Wanafunzi 34 waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi nchini wameondoka kwenda Ireland kwa ajili ya kuanza masomo ya shahada ya kwanza katika vyuo mbalimbali, kupitia mpango wa ufadhili wa Samia Scholarship Extended unaoratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Akizungumza wakati wa kuwaaga wanafunzi hao,leo Agost 28,2026 Airport Jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Silvia Lupembe alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kukabiliana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani.
Alisema kundi hilo ni sehemu ya mpango mpana ambao ulianza kwa kupeleka wanafunzi 16 nchini Afrika Kusini, ambako wanajifunza katika Chuo Kikuu cha Johannesburg, huku wanafunzi 34 waliobaki wakipelekwa Ireland kusoma katika vyuo mbalimbali, wakibobea katika maeneo ya data science, akili unde (artificial intelligence), mathematical sciences na taaluma nyingine zinazohusiana na sayansi na teknolojia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu wa Wizara hiyo, Profesa Steven Osward Maruka, alisema wanafunzi hao walichaguliwa kutokana na kuwa miongoni mwa waliofanya vizuri zaidi katika matokeo ya Kidato cha Sita na walipatiwa maandalizi maalumu kabla ya kuanza masomo yao ya shahada ya kwanza nchini Ireland.
Profesa Maruka alisema kabla ya kuondoka nchini, wanafunzi hao wamepitia mafunzo ya takribani miezi 10 katika kambi maalumu (boot camp), yaliyolenga kuwaandaa kitaaluma na kuwapa ujuzi wa kompyuta, programming, sayansi, pamoja na maandalizi ya namna ya kuishi na kusoma katika mazingira ya nje ya nchi.
Ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa Samia Scholarship tangu mwaka 2022/23 kwa kuwafadhili wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ndani ya nchi, huku mwaka huu ikiwa ni awamu ya kwanza kwa mpango huo kupanuliwa ili kuwawezesha wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kupata elimu katika vyuo vya nje ya nchi.
Mmoja wa wanufaika wa mpango huo, Angela Mongi, aliyemaliza Kidato cha Sita katika Shule ya St Mary’s Mazinde Juu, Tanga, alisema amepata nafasi ya kusoma Bachelor of Mathematical Sciences katika Chuo Kikuu cha Limerick nchini Ireland na kuahidi kutumia elimu atakayoipata kwa manufaa ya Tanzania.
Naye mwanafunzi mwingine, Rodgers Richard, aliyemaliza Kidato cha Sita katika shule ya boys ya Njombe, alisema nafasi hiyo imetimiza ndoto yake ya kupata elimu ya juu nje ya nchi, akiwataka vijana wengine kufanya vizuri katika masomo ili waweze kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali.
Hata hivyo mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, Sangaru Mainuka James, aliishukuru Serikali kwa kuwawezesha vijana hao kusoma taaluma zinazohusiana na teknolojia, akisema wataalamu watakaopatikana wanaweza kusaidia katika ujenzi wa mifumo ya kisasa katika sekta mbalimbali ikiwamo afya, kodi na huduma nyingine za umma. Wazazi wengine pia walieleza matumaini yao kuwa wanafunzi hao watatumia elimu watakayoipata kuleta mabadiliko na kuchangia maendeleo ya taifa.
Naye Prof Liliane Pasape Mratibu wa Programu-NMAIST amesema Wanafunzi hao waliandaliwa kwa hatua mbalimbali kabla ya kujiunga na vyuo vya nje, ikiwemo kuwawezesha kuomba nafasi za masomo na kufanya mitihani iliyowawezesha kupata udahili. Aidha, walipewa maandalizi maalumu kuhusu maisha ya ugenini, yakiwemo matumizi ya lugha, usimamizi wa fedha na namna ya kuendana na mazingira mapya ya masomo.
Mbali na maandalizi hayo, wanafunzi walipewa mafunzo ya matumizi ya kompyuta, programu na masuala ya mashindano ya kisayansi, huku wakipatiwa pia mafunzo ya uzalendo. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea kujiamini, kuipenda na kuiwakilisha Tanzania vyema wanapokuwa nje ya nchi, pamoja na kuwasaidia kuishi kwa nidhamu na kuzingatia wajibu wao kama wanafunzi na mabalozi wa nchi.


