Dodoma 

Wajumbe wa Bodi yaTaasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Menejimenti ya Taasisi, leo Agosti 28, 2026, wamekutana katika Ukumbi wa Mikutano wa Prof. Abdulkarim Mruma, uliopo katika Ofisi za GST, kwa ajili ya kujadili pamoja na mambo mengine mipango ya Taasisi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Kikao hicho kimejadili taarifa ya hesabu za GST, mipango na mikakati ya utekelezaji wa majukumu ya GST katika mwaka mpya wa fedha, kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuhakikisha Taasisi inafikia malengo yake ya kimkakati.

Akiongoza kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya GST, Bi. Yokobeth Myumbilwa, amewataka wajumbe wa Bodi kutoa maoni ya wazi na ushauri pale wanapoona kuna maeneo yanayohitaji maboresho, ili kuwezesha Taasisi kufanya kazi kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa.

Amesema hatua hiyo inaendana na maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo Agosti 27, 2026, ambapo aliwasihi wajumbe wa Bodi kuwa wabunifu na kuja na mawazo mapya yatakayosaidia kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi wa Taasisi.

Bi. Myumbilwa ameongeza kuwa Bodi na Menejimenti wanapaswa kuwa tayari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuleta matokeo makubwa, hususan katika utekelezaji wa Dira 2050.

Amesema juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa GST, Mhandisi Ally Samaje, amesema Taasisi imejiandaa kutekeleza mipango mbalimbali inayolenga kuongeza eneo la nchi lililofanyiwa utafiti wa kina wa jiofizikia kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 50 ifikapo 2030.

Hatua hizo zitasaidia kuongeza upatikanaji wa taarifa sahihi za rasilimali madini na kuchochea uwekezaji katika sekta hiyo.

Naye, Mjumbe wa Bodi ya GST, Dkt. Eva Shayo ameshauri utekelezaji wa mipango ya Taasisi, hususan katika maeneo ya fedha na manunuzi, kuzingatia ubora, ufanisi na thamani ya fedha.

Sambamba na hayo, Prof. Elisante Mshiu amesisitiza umuhimu wa GST kuhakikisha vifaa vinavyonunuliwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Taasisi vinakuwa vya kisasa, vipya na vinavyoendana na mahitaji ya sasa ya kiteknolojia, ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi.

Aidha, Bodi imeipongeza Menejimenti ya GST kwa namna ilivyojipanga kutekeleza mipango yake ya tafiti za madini nchini.

Kikao hicho ni sehemu ya hatua za GST katika kuimarisha usimamizi, uwajibikaji na utekelezaji wa mipango ya Taasisi, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utafiti wa jiolojia na madini na kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Taifa kupitia sekta ya madini.