LAWAMA ZA KISIASA HAZISHABIHIANI NA MAKUBWA YA RAIS SAMIA- MALOTO
UTENDAJI WA RAIS SAMIA UMEKUWA MWIBA KWA MAADUI ZAKE
Na Luqman Maloto
Mwandishi wa habari Luqman Maloto amesema historia inaweza kumweka huru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na matokeo ya miradi mikubwa ya maendeleo iliyotekelezwa na kukamilishwa katika kipindi cha uongozi wake. Maloto ametumia kauli ya mwanazuoni Peter Drucker kwamba uongozi madhubuti hupimwa kwa matokeo, si hotuba wala sifa.
Maloto ametumia kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) kama mfano mkuu, akisema Rais Samia alipokula kiapo Machi 19, 2021, mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 37, lakini hadi Agosti 22, 2026 ulikamilika kwa asilimia 100. Kwa mtazamo wake, Rais Samia alisimamia asilimia 63 iliyobaki ya utekelezaji wa mradi huo.
Amesema wakati wa utekelezaji wa JNHPP kulikuwa na mashaka kuhusu uwezo wa Rais Samia kukamilisha miradi mikubwa iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Magufuli, huku baadhi ya wakosoaji wakitoa kauli za wazi kwamba asingeweza. Hata hivyo, amesema Rais Samia hakujikita kujibu kwa maneno, bali aliruhusu kazi na matokeo kuzungumza.
Maloto amesema kukamilika kwa JNHPP kunapaswa kutazamwa pia katika historia ya muda mrefu ya wazo la kuzalisha umeme mkubwa katika Mto Rufiji, akibainisha kuwa utekelezaji wa mradi ulianza mwaka 2017 na jiwe la msingi likawekwa mwaka 2019. Ameongeza kuwa katika kipindi cha Rais Samia kulikuwa na mabadiliko kadhaa ya mawaziri wa Nishati, viongozi wa TANESCO na wahandisi wakazi wa mradi, jambo analoliona kama sehemu ya jitihada za kuhakikisha mradi unakamilika.
Akitumia falsafa ya Niccolò Machiavelli kwamba matokeo ya mwisho yanaweza kutoa hukumu kuhusu maamuzi yaliyofanyika, Maloto amesema muda umeanza kutoa majibu kuhusu mjadala wa JNHPP. Ameunganisha hoja hiyo na kauli maarufu ya Fidel Castro, “History Will Absolve Me” — “Historia Itaniweka Huru”, akisema historia mara nyingi hutoa hukumu tofauti na mijadala ya kisiasa ya wakati husika.
Mbali na JNHPP, Maloto ametaja miradi mingine kama upanuzi wa miundombinu ya mabasi ya mwendokasi Dar es Salaam, maendeleo ya reli ya Standard Gauge, kuanza kwa treni za umeme kati ya Dar es Salaam na Dodoma, pamoja na kukamilika kwa Daraja la Kigongo–Busisi, akisema yote yanaweza kuwa sehemu ya kumbukumbu ya utawala wa Rais Samia.
Kwa Maloto, presha za kisiasa na lawama zinazomkabili kiongozi akiwa madarakani si lazima ziwe hukumu ya mwisho ya historia. Amesema baada ya Rais Samia kuondoka madarakani, Watanzania watapata nafasi ya kuangalia nyuma na kutathmini matokeo ya utawala wake kwa upana zaidi, ndipo kazi iliyofanyika katika kipindi chake inaweza kutoa msingi wa historia kumtetea na kumweka huru.
