Mamlaka ya Elimu na Maunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na kampuni ya ushauri na utalaamu wa biashara na miradi (ASNL Advisory Limited), jana tarehe 27 Agosti 2026 wamefanya ziara ya pamoja katika mgodi wa Graphite Lindi Jumbo, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, kwa lengo la kujifunza teknolojia zinazotumika na ujuzi unaohitajika katika maeneo ya mgodi huo.

Mgodi wa Graphite Lindi Jumbo unachimba madini ya Kinywe (Graphite), ambayo hutumika kutengeneza betri za magari ya umeme (EVs) na paneli za umeme jua.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore amesema VETA imetambua teknolojia zinazotumika katika mgodi huo na hivyo kupata mawazo ya namna ya kuzitafsiri katika mafunzo kuzalisha wahitimu wanaoweza kuajirika katika mgodi huo na mingine yenye teknolojia kama hizo.

“Tumetambua tenkolojia zinazotumika katika mgodi huu kwenye shuguli za uzalishaji, nasisi tutakwenda kufundisha wanafunzi katika vyuo vyetu ili wanapohitimu waweze kupata ajira migodini,” amesema CPA Kasore.

Sambamba na hilo CPA Kasore amesema ziara hiyo imepelekea kuona haja yakuwa na 

ushirkiano rasmi (MoU) na mgodi huo, ili wakufunzi wajengewe uwezo zaidi kulingana na mahitaji ya soko la ajira, sambamba wanafunzi wa VETA kwenda mgodini kupata mafunzo kwa vitendo yanayo husu shughuli za uchimbaji madini.

CPA Kasore amesema, ”VETA tuna programu maalum ya kurasimisha ujuzi (RPL) na hapa 

Lindi Jumbo mnatoa mafunzo kwa vijana wanaozunguka eneo la mgodi ili na wao washiriki katika shughuli za uzalishaji hapa kama vile uchomeleaji na kuendesha mitambo, tunaona ipo haja ya sisi kuwafanyia tathmini na kubaini mapungufu waliyonayo kwenye ujuzi waliopata, kuziba hayo mapungufu na kwapatia vyeti kulingana na ujuzi walioupata hapa mgodini.”

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mgodi wa Graphite Lindi Jumbo, Makasi Saimon ameshauri mpango wa VETA kushirikiana na migodi uendelezwe kwa ukubwa zaidi ili vijana wanaohitimu katika vyuo vya VETA waweze kupata nafasi ya kufanya kazi katika migodi mbalimbali ili kuwa na mawanda mapana na matokeo makubwa kitaifa.

Aidha Mkurugenzi kutoka Kampuni ya ASNL, Humphrey Simba amesema wanashirikiana na VETA katika kujenga nguvukazi yenye ujuzi katika sekta ya madini, wao kama washauri wanaangalia ni ujuzi gani unahitajika katika sekta ya madini, hasa madini ya kimkakati na hiyo ndiyo sababu kuu ya ziara katika mgodi huo. 

Mourice Japhet ni mmoja wa wahitimu wa chuo cha VETA Moshi kupitia Mpango wa Mafunzo Ufundi Jumuishi kwa ajili ya Uchimbaji Madini (IMTT) ambaye ameajiriwa kwenye kitengo cha ufundi wa mitambo katika mgodi huo amesema, “ninajivunia sana mimi na wenzangu kama wazawa kufanya kazi hapa kwani hapo awali mafundi wengi migodini walitoka mataifa mengine lakini kwa sasa ni tofauti , ningeomba VETA iendelee kutoa mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha wazawa kufanya kazi katika miradi mbalimbali pamoja na migodini.”