Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha viuatilifu vinavyotumika nchini vinakuwa salama kwa wakulima, walaji na mazingira, ikiwemo kuondoa sokoni viuatilifu 205 vilivyobainika kuwa na viambata amilifu hatarishi.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 27,2026 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo wa mwaka 2026/2027, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kufanyika kwa tathmini ya kiafya na kimazingira.

Amesema Kuwa  viuatilifu 675 vimeondolewa kwenye orodha ya viuatilifu vilivyosajiliwa baada ya kushindwa kuhuisha usajili wake kwa zaidi ya miaka 10.

Aidha, amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, TPHPA ilikagua maduka 5,157 ya viuatilifu na kutoa vibali 3,831 vya kuingiza viuatilifu nchini.

 amebainisha Kuwa viuatilifu vipya 508 vilisajiliwa, huku sampuli 3,463 za viuatilifu zikichukuliwa na kufanyiwa uchambuzi wa kimaabara.

“Kati ya sampuli hizo, sampuli 132 sawa na asilimia nne hazikukidhi viwango na wahusika waliagizwa kurejesha shehena hizo,” ameseme Prof. Ndunguru

Katika kuimarisha udhibiti wa masalia ya viuatilifu kwenye chakula, Prof. Ndunguru amesema TPHPA imeanzisha mpango maalumu wa kuchukua sampuli za mazao ya chakula katika masoko ya mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.

Amesema mpango huo utafanyika kila mwaka kwa lengo la kuhakikisha mazao yanayowafikia wananchi yanakuwa salama kwa matumizi na hayahatarishi afya ya walaji wala mazingira.

Ameongeza Kuwa TPHPA  imewekeza shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya ununuzi wa mashine tano za kisasa za kuchambua ubora wa viuatilifu na masalia kwenye mazao ya chakula na mazingira.

Amesema mashine hizo tayari zimeanza kufanya kazi na zina uwezo wa kuchakata zaidi ya sampuli 2,000 kwa wiki.

Katika kuendelea kulinda afya ya wananchi, amesema mwaka wa fedha 2026/2027 TPHPA itaongeza ukaguzi wa viuatilifu, kudhibiti viuatilifu bandia na visivyosajiliwa pamoja na kuendelea kufanya tathmini ya viuatilifu kiafya na kimazingira.

Pia, mamlaka itaongeza elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu.

Pia amewataka wakulima kutumia viuatilifu vilivyosajiliwa na kufuata maelekezo ya wataalamu, akisisitiza kuwa matumizi holela ya viuatilifu yanaweza kuhatarisha afya ya binadamu, mazingira na masoko ya mazao ya Tanzania.