Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

WAZAZI na walezi katika Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, wametakiwa kutumia fursa ya kampeni ya chanjo ya Polio kuwakinga watoto wao dhidi ya ugonjwa huo, huku jamii ikihimizwa kushirikiana kikamilifu kufanikisha zoezi hilo.

Mkuu wa wilaya ya Kibaha Nickson John ametoa wito huo wakati akimwakilisha mkuu wa Mkoa wa Pwani, kuzindua kampeni ya chanjo ya matone ya Polio aina ya nOPV2 ,katika Kituo cha Afya Mkoani, iliyoanza kutolewa Agosti 27 hadi 30, mwaka huu .

Nickson amesema chanjo hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha watoto wanapata kinga dhidi ya Polio, hivyo wazazi wanapaswa kuwapeleka watoto wao kwenye vituo na maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya utoaji wa chanjo.

Ameeleza ushiriki wa kila mzazi ni muhimu kwa kuwa mtoto anaweza kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa huo endapo hatapata kinga inayohitajika, akiwataka wananchi kutopuuza kampeni hiyo.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Kusirye Ukio, ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Afya kwa maandalizi ya kampeni hiyo, akisema Mkoa umeanza vizuri na unaendelea na zoezi hilo hadi litakapokamilika katika halmashauri zote tisa.

Ukio amesema awamu ya pili ya kampeni hiyo inatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 2, mwaka huu, huku zaidi ya watoto 500,000 wenye umri chini ya miaka 10 wakitarajiwa kupatiwa chanjo hiyo Mkoa wa Pwani.