Na: OWM – TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Kata zenye uhitaji kwa kuzingatia kigezo cha wingi wa watu, umbali na ugumu wa kufikika vikiwemo vya Kata za Namhula, Chitengule, Igundu, Nansimo na Nampindi, ili kusogeza huduma za dharura na upasuaji karibu na wananchi.
Prof. Shemdoe amesema hayo leo, Agosti 27, 2026 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mhe. Kangi Lugola Mbunge wa Jimbo la Mwibara aliyetaka kujua ni lini Serikali itajenga Vituo vya Afya katika Kata za Butimba, Nyamihyolo, Namhula, Chitengule, Igundu, Nansimo na Nampindi.
“Mhe. Spika, ukiacha Kata ya Butimba na Nyamihyolo, Kata za Namhula, Chitengule, Igundu, Nansimo na Nampindi zote zina wakazi zaidi ya 10,000 na hivyo kukidhi vigezo vya kujengewa Kituo cha Afya. Aidha, Kituo cha Afya Chitengule ni moja kati ya vituo vya Afya vya kimkakati 94 ambavyo fedha yake tayari OWM – TAMISEMI imeiomba Wizara ya Fedha,” amefafanua Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe ameeleza kuwa, vituo vingine vilivyobaki vya Namhula, Igundu, Nansimo na Nampindi vimewekwa kwenye mpango wa ujenzi, fedha zitakapopatikana zitapelekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa ajili ya ujenzi na kuongeza kuwa mara baada ya kikao cha Bunge kumalizika atakwenda Jimbo la Mwibara kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa ujenzi wa vituo vya afya jimboni humo.
Alipopewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, Mhe. Lugola amesema kuwa ameridhishwa na majibu mazuri ya Serikali ambayo yameleta matumaini kwa wananchi wa Mwibara, hivyo hana swali lolote la nyongeza na badala yake alimpongeza Prof. Shemdoe kwa utendaji kazi mzuri unaoendana na maono na kasi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za kijamii.
“Nina amini Mhe. Waziri Prof. Shemdoe ni miongoni mwa mawaziri wanayoyaishi maneno yao kwa vitendo ili kuendana na azma na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea watanzania maendeleo,” amesema Mhe. Lugola.
Prof. Shemdoe amejibu maswali mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na ya nyongeza wakati wa Kikao cha Pili cha Mkutano wa Nne wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

