Na S’SGT. Ponsiano Lindi – DSM
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amempongeza Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, kwakazi kubwa anayoifanya katika kuleta mabadiliko ndani ya Jeshi la Magereza, akieleza kuwa ni miongoni mwa viongozi wachache waliofanikiwa kuleta mabadiliko ndani ya muda mfupi.
Mhe. Mpogolo, ametoa pongezi hizo, Agosti 27, 2026, wakati akishiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la Kambi ya Magereza Mvuti, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
“Natoa pongezi za dhati kabisa kwa Jeshi la Magereza kwa kubuni na kuanzisha Kampeni ya “Magereza Nuru ya Mabadiliko”, kwa kushirikiana na TBC, ni kampeni muhimu katika kuufahamisha umma kuhusu kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Magereza katika kuwabadilisha wafungwa na kuwaandaa kurejea katika jamii wakiwa raia wema na wenye tija” amesema Mhe. Mpogolo
Aidha, Mhe. Mpogolo, amesema Jeshi la Magereza lina uwezo wa kubadilisha maisha ya wafungwa kupitia programu mbalimbali za urekebishaji, ikiwemo kuwafundisha kusoma na kuandika, kushona, ufundi umeme, teknolojia na stadi nyingine za maisha.
Kwa upande wake, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP. Nicodemus Tenga, amesema Jeshi la Magereza limejiwekea mkakati wa kushirikiana na TBC katika kuzifikisha kwa jamii kazi zinazofanywa na Jeshi kupitia Kampeni ya mwezi mmoja ya Magereza Nuru ya Mabadiliko.
CP Tenga amesema zoezi la upandaji miti lililofanyika katika Kambi ya Magereza Mvuti limefanikisha upandaji wa zaidi ya miti 800, huku akisisitiza kuwa miti hiyo itatunzwa na kuhakikisha inakua na kuleta manufaa kwa jamii na mazingira.
Amesema utunzaji wa mazingira ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, huku akieleza kuwa ajenda ya upandaji miti, utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa misitu ndani ya Jeshi la Magereza ni miongoni mwa vipaumbele.
Katika hatua nyingine, CP. Tenga, ametoa rai kwa jamii kuona umuhimu wa kuwapokea wafungwa wanaomaliza vifungo vyao, akieleza kuwa itawasaidia kuto rejea katika uhalifu na kurudi magerezani.

