*Ampongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuiwezesha Sekta ya Madini katika Utafiti

DODOMA 

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imetakiwa kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika utafiti wa madini na tafiti za jiosayansi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, kupitia uwekezaji mkubwa katika teknolojia, wataalamu, miundombinu na upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiolojia.

Hatua hiyo inaenda sambamba na mkakati wa Serikali wa kuongeza kiwango cha tafiti za kina za madini nchini ili kubaini maeneo mapya yenye rasilimali za madini, kuongeza uwekezaji na kupunguza utegemezi wa uchimbaji wa kubahatisha.

Rai hiyo imetolewa leo Agosti 27, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Madini *Mhe. Anthony Mavunde* wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya GST, ambapo amesema kuwa katika kulipeleka taifa katika uchumi wa dola trilioni moja, GST inatakiwa ifanye utafiti wa jiolojia katika kilomita za mraba 50,000 ndani ya Quarter Degree Sheet (QDS) 20 ambazo sawa na asilimia 5 ya nchi nzima.

Aidha, Waziri Mavunde ameitaka Bodi ya GST kufanya utafiti wa kina katika idadi ya QDS 23 kwa lengo la kuongeza taarifa mpya za rasilimali madini nchini kutoka asilimia 16 zilizopo sasa hadi 21 ifikapo mwaka 2030.

Waziri Mavunde ameielekeza Bodi ya GST kuhakikisha kuwa, wataalam wa GST wanatumia mifumo ya teknolojia ya kisasa katika utunzaji wa taarifa za jiosayansi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani yanayowezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na usahihi.

Kwa upande wake, Naibu waziri wa Madini *Dk. Steven Kiruswa* ameitaka GST kufanya shughuli zake za utafiti kwa kushirikiana kwa ukaribu na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili kuendelea kubaini maeneo mapya yenye madini katika nchi na kuendeleza maeneo ambayo tayari yana taarifa za upatikanaji wa madini.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, *Bw. Msafiri Mbibo* amesema katika kipindi cha miaka 100 GST imefanikiwa kufanya mambo makubwa katika sekta ya madini, hivyo kupitia Bodi hiyo ana matumaini makubwa hususan kwenye kutatua changamoto mbalimbali zitakazosaidia kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini na kuvutia wawekezaji.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi, *Bi. Yokobeth Myumbilwa* ameishukuru serikali kwa kuridhia kutengwa kwa asilimia 10 itokanayo na makusanyo ya madini ili fedha hizo zitumike kwa shughuli za utafiti wa madini nchini ili kuongeza taarifa mpya zitakazosaidia kukuza sekta ya madini kiuchumi.

Mtendaji mkuu wa GST, *Mha. Ally Samaje* amesema watumishi wa taasisi pamoja na Menejimenti wapo tayari kushirikiana na bodi hiyo katika utendaji wa majukumu yao ili kufanikisha malengo ya taasisi katika kuhudumia watanzania kupitia shughuli za utafiti wa Madini na utoaji wa taarifa za Jiosayansi.