Na Silivia Amandius.
Kagera.
Mkoa wa Kagera umejiandaa kuupokea Mwenge wa Uhuru utakaofika mkoani humo Agosti 30, 2026, ukitokea Mkoa wa Geita. Mwenge huo utaanza mbio zake katika Wilaya ya Muleba, katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Nyakabango, na utatumia jumla ya siku nane katika mkoa huo.
Katika kipindi hicho, Mwenge wa Uhuru utafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuzindua, kuweka mawe ya msingi, kufungua na kukagua miradi 54 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi 23,074,953,103. Miradi hiyo inatekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera na inalenga kuchochea maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.
Taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera inaeleza kuwa kati ya miradi hiyo, 25 itawekewa mawe ya msingi, mitano itafunguliwa, 11 itazinduliwa na miradi 13 itatembelewa na kukaguliwa. Sekta zitakazonufaika ni pamoja na afya, elimu, maji, mazingira, ujasiriamali, uwezeshaji wa vijana na uwekezaji.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 zinafanyika chini ya kaulimbiu “Tanzania ni Yetu Sote, AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO WA KITAIFA, Tushikamane kwa Pamoja Kuletea Maendeleo.” Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha wananchi kudumisha amani, umoja na mshikamano, huku wakielimishwa kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, malaria, VVU/UKIMWI, dawa za kulevya na umuhimu wa lishe bora.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi na shughuli za Mwenge wa Uhuru, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuendelea kuhamasisha maendeleo na mshikamano wa jamii. Mwenge huo unatarajiwa kuhitimisha mbio zake mkoani Kagera Septemba 6, 2026, kabla ya kukabidhiwa Mkoa wa Kigoma siku inayofuata.

