Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania (JWTZ) , Luteni Jenerali Salum Haji Othman, akizungumza katika uzinduzi Wiki ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiraia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) itakayofanyika nchini Tanzania leo Agosti 26, 2026 katika viwanja vya Golf Lugalo jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sita ya Ushirikiano wa Majeshi ya Afrika Mashariki 2026, Brigedia Jenerali Dkt. Agatha Mary Katua ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Utawala wa JWTZ akifafanua baadhi ya mambo yatakayofanyika kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la wanannchi wa Tanzania JWTZ Luteni Jenerali Salum Haji Othman ili kuzindua wiki hiyo. 

…………….

Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Luteni Jenerali Salum Haji Othman, amesema kufanyika kwa Wiki ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiraia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) nchini Tanzania kwa mara ya pili ni ushahidi wa kiwango cha juu cha imani na uaminifu uliowekwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema JWTZ linatoa shukrani kwa majeshi yote yanayoshiriki katika shughuli hiyo, huku akiwapongeza Wakuu wa Majeshi na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa dhamira yao ya kuendeleza na kuimarisha mchakato wa ujumuishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia shughuli za pamoja za ulinzi na usalama.

Luteni Jenerali Othman amesema ushirikiano huo umekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha Wiki ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiraia ya EAC tangu toleo lake la kwanza lililofanyika nchini Uganda mwaka 2020, huku toleo la sita likiandaliwa kwa kuzingatia uzoefu na mafanikio ya matoleo yaliyotangulia.

Kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob John Mkunda, pamoja na familia nzima ya JWTZ, ametoa shukrani kwa viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, wajumbe wa majeshi rafiki na wageni wote walioshiriki katika tukio hilo, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kwa manufaa ya wananchi wa Afrika Mashariki.

Amesema Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC, Baraza la Kisekta la Ulinzi na Usalama pamoja na Kamati ya Ushirikiano katika Masuala ya Ulinzi wamekuwa wakitoa mwongozo wa kimkakati, msaada na fursa kwa majeshi ya nchi wanachama kufanya kazi kwa pamoja.

Aidha, Luteni Jenerali Othman amewakaribisha wageni kutoka majeshi rafiki na kuwaambia wajisikie nyumbani nchini Tanzania, kabla ya kutangaza rasmi uzinduzi wa toleo la sita la Wiki ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiraia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sita ya Ushirikiano wa Majeshi ya Afrika Mashariki 2026, Brigedia Generali JWTZ Agatha Katua, amesema tukio hilo ni kilele cha miezi kadhaa ya maandalizi, mipango na uratibu kati ya nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema shughuli hizo zitahusisha utoaji wa huduma za afya bure, misaada ya kibinadamu pamoja na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya, zikiwa na lengo la kuimarisha uhusiano kati ya raia na jeshi katika nchi wanachama wa EAC.

Brigedia Generali Katua amesema zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa Ibara ya 2 na 9 ya Itifaki ya EAC kuhusu Ushirikiano katika Masuala ya Ulinzi, pamoja na uamuzi Na. 38 wa kikao cha 41 cha Baraza la Kisekta la Ushirikiano katika Masuala ya Ulinzi kilichofanyika Nairobi.

Amesema shughuli hizo pia zimeunganishwa katika Mpango wa JWTZ wa Kuwafikia Wananchi katika Masuala ya Ulinzi na Usalama wa Tanzania wa mwaka 2026, hatua inayolenga kuongeza manufaa ya zoezi hilo kwa jamii na kuonesha nafasi ya majeshi katika maendeleo ya taifa, ujenzi wa amani na ustahimilivu wa jamii.

Ameeleza kuwa vikosi kutoka Burundi, Kenya, Rwanda, Somalia na Uganda vitashiriki katika shughuli hizo, ambazo zitafanyika Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Pemba na Unguja, pamoja na maeneo mengine kupitia timu za huduma za afya zinazokwenda moja kwa moja katika jamii.

Brigedia Generali Katua amesema huduma za afya zitatolewa katika hospitali na vituo vilivyochaguliwa, huku shughuli nyingine zikijumuisha ukarabati mdogo wa vituo vya afya na utoaji wa misaada ya kibinadamu katika vituo vya watoto yatima, magereza na vituo vya watu wenye mahitaji maalumu.

Amesema shughuli hizo zitaanza Agosti 26, 2026 na kufikia tamati Septemba 1, 2026, ambapo hafla ya kufunga itaambatana na maadhimisho ya miaka 62 ya JWTZ, lililoanzishwa Septemba 1, 1964, pamoja na burudani na chakula cha jioni cha gala.

Ameishukuru Kamati ya Maandalizi, timu za madaktari, wahandisi, wapangaji na wadau wengine kwa kufanikisha maandalizi ya zoezi hilo, huku akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua shughuli hizo na kupokea vifaa tiba vitakavyotumika katika utoaji wa huduma za afya bure pamoja na vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya vilivyochaguliwa.