DODOMA, Agosti 26, 2026

Tume ya Madini imetoa muda wa siku 30 kwa wamiliki na wawezeshaji wa miradi ya uchimbaji mdogo yenye Mikataba ya Msaada wa Kiufundi kurekebisha mapungufu yaliyobainika wakati wa ukaguzi, ikionya kuwa itachukua hatua za kisheria, ikiwemo kufuta ridhaa za Msaada wa Kiufundi, kwa watakaoshindwa kutekeleza matakwa hayo.

Hatua hiyo inahusu miradi 128 iliyofanyiwa ukaguzi na Tume ya Madini, ambapo miradi 42 ilibainika kutofanya kazi na mingine 86, licha ya kuwa inaendelea na shughuli za uchimbaji, ilibainika kuwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli zake na uzingatiaji wa masharti ya Mikataba ya Msaada wa Kiufundi.

Akizungumza jijini Dodoma leo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema Tume imetoa Hati za Makosa zenye muda wa siku 30 kwa wamiliki wa miradi 42 iliyobainika kutofanya kazi, ili watoe mrejesho wa hatua walizochukua kurejesha utekelezaji wa shughuli zao kwa mujibu wa sheria na masharti ya ridhaa za Msaada wa Kiufundi.

Amesema ukaguzi huo ulifanyika kufuatia maelekezo ya Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, yaliyotolewa Aprili 27, 2026, wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Kwa mujibu wa Mhandisi Lwamo, miongoni mwa changamoto zilizobainika katika miradi inayofanya kazi ni pamoja na kutotekelezwa ipasavyo kwa mipango inayotakiwa kisheria, ikiwemo Mpango wa Usimamizi wa Mazingira ulioidhinishwa, Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), Mpango wa Uhawilishaji wa Teknolojia, Mpango wa Uchimbaji na Mpango wa Ufunguaji wa Mgodi.

Aidha, amesema wamiliki wa miradi 86 inayofanya kazi lakini yenye mapungufu, pamoja na wawezeshaji wa Msaada wa Kiufundi, wanatakiwa kurekebisha kasoro hizo ndani ya siku 30 kwa mujibu wa Kanuni za Msaada wa Kiufundi kwa Wamiliki wa Leseni Ndogo za Uchimbaji Madini za Mwaka 2025.

“Endapo wahusika wa miradi hiyo watashindwa kutekeleza matakwa yaliyowekwa ndani ya muda huo, Tume ya Madini itachukua hatua zaidi za kisheria, ikiwemo kufuta ridhaa za Msaada wa Kiufundi,” amesema Mhandisi Lwamo.

Amesema Tume itaendelea kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara katika miradi inayotekelezwa kupitia Msaada wa Kiufundi, kwa lengo la kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Madini, kanuni zake na masharti ya ridhaa zilizotolewa.

Wakati huo huo, Mhandisi Lwamo amewataka wanufaika wa Msaada wa Kiufundi pamoja na wachimbaji wadogo wa madini kuendelea kuzingatia matakwa ya utunzaji wa mazingira, usalama na afya mahali pa kazi.

Amesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari zaidi katika shughuli za uchimbaji, hususan katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na tahadhari kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mvua za El Niño, ili kulinda usalama wa wachimbaji, mali na mazingira yanayozunguka maeneo ya migodi.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Tume ya Madini za kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya uchimbaji mdogo, kuhakikisha Msaada wa Kiufundi unatolewa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, sambamba na kuongeza tija, usalama na uendelevu wa shughuli za uchimbaji madini nchini.