Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Onesmo Mbise akizungumza mbele ya Waziri wa madini kuhusu changamoto.zinazowakabili
Happy Lazaro,Manyara.
Manyara .Kampuni ya Franone Mining & Gems Ltd imeeleza kuwa kuendelea kupungua kwa uzalishaji wa Tanzanite katika eneo la Mererani kunahitaji Serikali na wadau wa sekta ya madini kuongeza nguvu katika tafiti za kina ili kubaini mikondo mipya ya madini hayo.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Onesmo Mbise, amesema changamoto hiyo imejitokeza baada ya maeneo yaliyokuwa yakizalisha Tanzanite katika hatua za awali kuanza kupungua, hali iliyosababisha shughuli za uchimbaji kuelekezwa zaidi kwenye maeneo ya chini ya ardhi.
Akizungumza mbele ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, Mbise amesema mazingira mapya ya uchimbaji yanahitaji utafiti wenye teknolojia na utaalamu zaidi ili wachimbaji waweze kufahamu kwa usahihi maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuwa na Tanzanite.
Amesema kwa sasa kampuni hiyo inaendelea kufuatilia mikondo ya chini ya ardhi, lakini mafanikio ya shughuli hizo yanategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiolojia zitakazosaidia kuelekeza uchimbaji katika maeneo yenye tija.
Mbise amesema Serikali tayari imechukua hatua kwa kutoa maelekezo ya kufanyika kwa utafiti zaidi katika eneo la Mererani, hatua ambayo anaamini inaweza kuwa mwanzo wa kupata maeneo mapya yatakayosaidia kurejesha kasi ya uzalishaji wa Tanzanite.
Kwa mujibu wa Mbise, timu maalumu tayari imeundwa chini ya uongozi wa Kamishna wa Madini, Dk. Mwanga, kwa ajili ya kushughulikia suala hilo, huku kampuni hiyo ikiahidi kushirikisha wataalamu wake katika mchakato huo.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali na kampuni zinazojihusisha na uchimbaji ni muhimu katika kutafuta majibu ya changamoto zinazojitokeza kwenye sekta hiyo, hasa katika kipindi ambacho shughuli za uchimbaji zinahitaji teknolojia na utafiti wa hali ya juu.
“Tutatoa utaalamu wetu na kuhakikisha tunashiriki pamoja ili tupate ufumbuzi na hali irudi kama kawaida,” amesema Mbise.
Ameeleza kuwa matokeo chanya ya utafiti yanaweza kufungua fursa mpya za uchimbaji, kuongeza uzalishaji wa Tanzanite na kuifanya sekta hiyo kuendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa Serikali na ajira kwa wananchi.
