Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

Agosti 26, 2026

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, amewasihi vijana wa Kata ya Tangini na jimbo hilo kujikita katika shughuli za kiuchumi na kutumia fursa zilizopo, ili kujiandaa na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inayolenga uchumi unaoongozwa na sekta binafsi.

Koka ameeleza, vijana wanapaswa kukimbilia fursa za kiuchumi, ikiwemo mikopo na elimu ya ujuzi mbalimbali, ili kuwawezesha kujiimarisha kiuchumi na kujenga maisha yao ya baadaye.

Koka ameyasema hayo wakati akifunga Baraza la Vijana la UVCCM Kata ya Tangini, lililojadili masuala ya kiuchumi, ikiwemo kufungua Shina la Wakereketwa wa Umoja wa Bodaboda (UWB) Tawi la NIDA na mradi wa uoshaji magari (car wash), pamoja na kujadili changamoto zinazokabili ofisi ya jumuiya hiyo.

Aidha amefafanua Serikali imeendelea kuweka fedha kwa ajili ya mikopo kwa vijana na makundi maalum, hivyo ni wajibu wao kuchangamkia fursa hizo na kuzitumia kubadili maisha yao.

Hata hivyo Koka amesema ,vijana ni taifa la leo na kesho, huku akieleza kuwa UVCCM ni sehemu ya kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora wa kisiasa, kitaifa na kiuchumi wenye nidhamu na maadili.

“Vijana wengi wanafeli kwa kukosa nidhamu, hata ukiwa umesoma, ukiwa na pesa, kama ukikosa nidhamu kwa wanaokusimamia na viongozi wako, huwezi kupata yote hayo, vijana wawe na nidhamu ya kujifunza na kuheshimu mamlaka,” anasisitiza Koka. 

Amewataka vijana kutoruhusu madaraka na fedha kuwabadilisha, hasa wale wenye ndoto za kufika mbali katika siasa, akiwatahadharisha kutokubali kutumika na watu wachache kwa kudanganywa kupewa ‘connection’.

Vilevile, Koka ametoa shilingi milioni moja kwa Shina la Wakereketwa wa Umoja wa Bodaboda (UWB) Kata ya Tangini, huku akiwataka madereva hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu ili kuepuka vikwazo vya kisheria.

Kwa upande wake, akimwakilisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani, Alhaji Hussein Chuma, Nassoro Shomvi amesema mjumbe huyo ameahidi kufanikisha kukamilishwa kwa ofisi ya jumuiya hiyo katika Kata ya Tangini.

Mwenyekiti wa CCM ambae pia ni Diwani wa Kata ya Tangini, Antony Milao, amebainisha baraza hilo linapaswa kuwa mfano kwa vijana wengine, huku akitoa rai kwa vijana kutumia mitandao ya kijamii, ikiwemo WhatsApp, Instagram na Facebook, kwa ajili ya kukisemea chama na kutafuta fursa badala ya kutumia muda mwingi kwa masengenyo na kupigisha shoti. 

Naye Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Joel Kituu, amesema UVCCM ni jumuiya inayohitaji kushikwa mkono ili kujijenga na kuendelea kuwaandaa vijana kwa majukumu ya baadaye.

Katibu wa UVCCM Kata ya Tangini, Lazaro Benjamin, amesema mradi wa uoshaji magari utasaidia kujiimarisha kiuchumi, lakini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kuendesha mradi huo, samani za ofisi pamoja na maboresho madogo yaliyobaki ili ofisi hiyo ianze kutumika kikamilifu.