Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Ngeleja Kadonya, amesisitiza umuhimu wa miradi inayotekelezwa chini ya usimamizi wa Bonde la Ziwa Victoria kuendelea kuleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi, hususan katika kuongeza kipato, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira.

Bw. Kadonya ameyasema hayo Agosti 25, 2026 wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, wakati wa ziara yake ya kujifunza na kupata taarifa kuhusu utekelezaji na matokeo ya miradi mbalimbali inayohusiana na Bonde la Ziwa Victoria.

Katika ziara hiyo, ametembelea miradi inayotekelezwa katika Kijiji cha Ng’haya, ikiwemo ufugaji wa kondoo, kilimo cha choroko, vitalu na upandaji miti pamoja na shughuli za ufugaji nyuki, ambayo ni sehemu ya jitihada za kujenga uwezo wa jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi sambamba na kuanzisha vyanzo endelevu vya kipato.

Akizungumza baada ya kujionea utekelezaji wa miradi hiyo, Bw. Kadonya amesema ni muhimu kuhakikisha uwekezaji unaofanyika kupitia programu na taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na unaendelea kuwa endelevu hata baada ya muda wa utekelezaji wa miradi kumalizika.

“Tunataka kuona miradi hii haibaki kuwa shughuli za muda mfupi, bali inajenga uwezo wa wananchi, inaongeza kipato cha kaya na wakati huo huo inalinda mazingira na rasilimali za Bonde la Ziwa Victoria. Matokeo yanayopatikana hapa Magu ni muhimu pia katika kutathmini manufaa ya ushirikiano wetu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Bw. Kadonya.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa wakati wa ziara hiyo, Mradi wa Majaribio wa Kikanda wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Bonde la Ziwa Victoria (ACC-LVB) umelenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga uwezo wa jamii kupitia usimamizi endelevu wa maji, kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa mifumo ya ikolojia.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni kuwezesha vikundi vya wananchi kujihusisha na shughuli za uzalishaji, ambapo vikundi vinne vya ufugaji wa kondoo vilivyowezeshwa kwa kondoo 160 mwaka 2023 vimeongeza idadi hiyo hadi kondoo 288, sambamba na utekelezaji wa shughuli za kilimo cha choroko, ufugaji nyuki na uzalishaji wa miche ya miti.