Na Hassan Kimweri, WAF – Addis Ababa

Tanzania imeendelea kusisitiza ushirikiano wa Umoja wa Afrika (AU) katika kuimarisha juhudi za kupunguza vifo vya mama na mtoto barani Afrika, hususan kupitia utekelezaji wa mikakati na hatua madhubuti zinazolenga kuboresha afya na ustawi wa makundi hayo.

Hayo yameongelewa leo Agosti 25, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe alipofanya kikao na Kamishna wa Afya, Masuala ya Kibinadamu na Maendeleo ya Jamii wa Tume ya Umoja wa Afrika Mhe. Balozi Amma Twum-Amoah, pembezoni mwa Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani (WHO-AFRO), unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Dkt. Magembe amemshukuru Mhe. Balozi Amma Twum-Amoah na Tume ya Umoja wa Afrika kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa kwa Tanzania katika sekta ya afya, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano huo ili kukabiliana na changamoto za afya na kuharakisha hatua za kupunguza vifo vya mama na mtoto barani Afrika.

Aidha, Dkt. Magembe amepongeza imani kubwa iliyowekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumfanya kuwa kinara wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Umoja wa Afrika akieleza kuwa nafasi hiyo ni fursa muhimu ya kuhamasisha dhamira na hatua za pamoja za viongozi wa Afrika katika kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amesema kuwa Tanzania iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya uzinduzi wa Mpango Mkakati wa utekelezaji (Roadmap) ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, unaotarajiwa kufanyika Arusha Septemba 9, 2026, na amemwalika Mhe. Balozi Amma Twum-Amoah kushiriki katika maandalizi na uzinduzi huo. 

“Lakini pia, tunaomba ushirikiano wa Tume ya Umoja wa Afrika katika maandalizi ya Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Viongozi wa Nchi na Serikali kuhusu Uhai wa Mama na Mtoto Barani Afrika, utakaofanyika Jijini New York Septemba 23, 2026, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,” amesema Dkt. Magembe