Na Hassan Kimweri, WAF – Addis Ababa

Tanzania imeunga mkono juhudi za kuimarisha Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia maboresho ya Muundo wa Mfumo wa Afya Duniani (Global Health Architecture), huku ikisisitiza umuhimu wa WHO kuendelea kutekeleza jukumu lake la msingi kama mamlaka ya kiufundi ya afya duniani. 

Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi, amesema hayo leo Agosti 25, 2026 kwenye Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani (WHO-AFRO), unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

“Tanzania inapongeza uongozi wa WHO katika kuratibu ushiriki wa Kanda ya Afrika kwenye utekelezaji wa marekebisho ya Kanuni za Kimataifa za Afya (International Health Regulations – IHR 2024) pamoja na kukamilishwa kwa viambatisho vyake katika Mkataba wa WHO,” amesema Dkt. Samizi 

Aidha, Dkt. Samizi amesema Tanzania inatambua mchango wa WHO katika kutoa msaada wa kiufundi ili kuimarisha mifumo ya afya, kuboresha ufuatiliaji wa magonjwa, kukabiliana na milipuko, kuendeleza huduma jumuishi za afya kwa wote pamoja na kuboresha afya ya mama na mtoto pamoja na vijana.

Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na WHO, taasisi za kikanda, washirika wa maendeleo na nchi wanachama katika kujenga mifumo ya afya imara, yenye usawa na inayomlenga mwananchi. 

Pai, Dkt. Samizi amesema Tanzania imedhamiria kukabiliana na changamoto za magonjwa yanayojitokeza na kuibuka upya, mabadiliko ya tabianchi, usugu wa vimelea dhidi ya dawa pamoja na upungufu wa rasilimali.