NA DENIS MLOWE IRINGA 

 

MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali yameendelea kuwa nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, yakishirikiana na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za afya, elimu, maji, kilimo, mifugo, miundombinu, uchumi wa kaya na ustawi wa jamii.

 

Hayo yameelezwa katika Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Wilaya ya Mufindi lililofanyika katika Ukumbi wa Mbalamaziwa, likiwakutanisha viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, madiwani, wenyeviti wa vijiji, wananchi, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

 

Wilaya ya Mufindi ina jumla ya mashirika 68 yaliyosajiliwa, ambapo 65 yanaendelea na shughuli zake katika mwaka wa fedha 2025/2026, mashirika hayo yameelezwa kuwafikia zaidi ya wananchi 48,000 kupitia utekelezaji wa afua mbalimbali za maendeleo.

Mchango wa mashirika hayo pia umeonekana katika uwekezaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo, ambapo kwa pamoja yanakadiriwa kuchangia zaidi ya Sh bilioni 15 kwa mwaka katika shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya wilaya hiyo.

 

Akizungumza katika jukwaa hilo, Mwenyekiti wa NaCoNGO Wilaya ya Mufindi, Fidelis Filipatali, amesema pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na mashirika hayo, kuna umuhimu wa kujenga mifumo itakayowezesha shughuli za mashirika kuendelea kuwa endelevu hata baada ya ufadhili wa miradi kumalizika.

 

Amesema kaulimbiu ya jukwaa hilo, “Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani,” inalenga kuyahamasisha mashirika kubuni vyanzo vipya vya mapato na kupunguza utegemezi mkubwa kwa wafadhili.

 

Filipatali amesema, mashirika yanapaswa kuwa na mifumo ya kuzalisha mapato huku yakizingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha, hatua ambayo itasaidia kulinda uendelevu wa miradi na kuongeza uwezo wa taasisi hizo kuwahudumia wananchi.

 

“Fikra mpya kuhusu maendeleo ya mashirika yasiyo ya kiserikali zinapaswa kutupeleka kwenye ubunifu, kujenga ubia na kutafuta vyanzo vya ndani vya fedha ili kuhakikisha miradi yetu inaendelea kuwa na manufaa kwa wananchi hata pale ufadhili unapomalizika,” amesema Filipatali.

 

Amesema NaCoNGO Mufindi itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sambamba na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

 

Filipatali pia amesema Mufindi imeanza kubadili mfumo wa uratibu wa shughuli za mashirika kwa kupunguza utegemezi wa mikutano ya ofisini na kuongeza ziara za kutembelea miradi moja kwa moja katika maeneo inakotekelezwa.

Amesema ziara hizo zinahusisha viongozi kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa hadi wilaya, pamoja na madiwani, jambo linalowezesha Serikali na wadau kuona hali halisi ya miradi, kutambua mafanikio na kubaini changamoto zinazohitaji ufumbuzi.

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dr.. Linda Selekwa, amesisitiza umuhimu wa mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akihimiza uwazi, uwajibikaji na uratibu mzuri wa shughuli zao.

 

Amesema ushirikiano kati ya Serikali na mashirika ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi na miradi inayotekelezwa inakwenda sambamba na mahitaji halisi ya wananchi.

 

Katika jukwaa hilo, mashirika mbalimbali yameendelea kuonesha namna yanavyoshiriki katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya maji, elimu, afya, kilimo, mifugo na uwezeshaji wa kiuchumi.

 

Filipatali, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Rural Development Organization (RDO), amesema shirika hilo pekee linachangia zaidi ya Sh bilioni 3 kwa mwaka katika miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Mufindi, ikiwemo sekta ya maji na elimu.

 

Amesema mchango huo ni sehemu ya jitihada za mashirika mbalimbali yanayofanya kazi wilayani humo, ambayo kwa pamoja yamekuwa yakichangia zaidi ya Sh bilioni 15 kwa mwaka katika shughuli za maendeleo.

 

Jukwaa hilo pia limetoa nafasi kwa mashirika makubwa na madogo kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhisho la pamoja, huku msisitizo ukiwekwa katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo endelevu kwa wananchi wa Mufindi.