MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, akizungumza na viongozi pamoja na wanachama wa CCM mkoani Singida katika Viwanja Vya Stendi ya Zamani wakati akihitimisha Zara yaka ya kikazi ya Siku 3 dani ya mkoa huo tarehe 21, 08,2026

…………………

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema CCM inalenga kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia saba ifikapo mwaka 2030, huku ukichochea ongezeko la kipato na kuboresha maisha ya wananchi.

Wasira amesema hayo (Agosti 21,2026) wakati akizungumza na viongozi pamoja na wanachama wa CCM mkoani Singida, akieleza kuwa ukuaji wa uchumi hautakuwa na maana iwapo hautaonekana katika maisha ya mtu mmoja mmoja kupitia ongezeko la kipato na fursa za kiuchumi.

Amesema katika Ilani ya CCM, chama hicho kimeweka msisitizo wa kukuza uchumi jumuishi unaolenga kumwezesha kila Mtanzania kunufaika na ukuaji wa uchumi.

“Katika Ilani yetu tumesema tunataka uchumi mkuu ambao kila siku mnasikia Tanzania uchumi wako unakuwa kwa asilimia 6.3. Lakini hii haitoshi. Tunataka uchumi huu usaidie maisha ya mtu mmoja mmoja,” amesema Wasira.

Ameeleza kuwa CCM inalenga kuona mapato ya wananchi yanaongezeka, huku akitolea mfano wakulima wa alizeti mkoani Singida ambao, kwa mujibu wake, wana nafasi kubwa ya kuongeza kipato kupitia kilimo na uwekezaji katika viwanda vya kuchakata zao hilo.

Wasira amesema Serikali imeweka hatua mbalimbali, ikiwamo kuongeza kodi kwa mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje, kwa lengo la kuwahamasisha wakulima wa alizeti kuongeza uzalishaji na hivyo kuongeza mapato.

Amesema hatua hiyo pia inalenga kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kusindika alizeti, ambavyo vitaongeza thamani ya zao hilo na kutoa ajira kwa wananchi.

“Nyinyi hapa ni wakulima wakubwa sana wa alizeti. Tumeweka kodi zaidi kwa mafuta yanayotoka nje ili kuwatia moyo watu wa Singida na mikoa inayolima alizeti waweze kulima zaidi, waongeze mapato, tuweke viwanda, viajiri watu, halafu maisha yaendelee kufanya nini? Kupanda,” amefafanua.

Kwa mujibu wa Wasira, dhamira hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya uchumi jumuishi inayolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya kuongeza kipato na kuboresha maisha yake.

Amesema dira hiyo pia imeainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo tayari imeanza kutekelezwa kwa kuweka msingi wa maendeleo yanayolenga kuifikisha Tanzania katika uchumi unaozalisha fursa kwa wananchi wengi zaidi.

Ameeleza kuwa wanaodai kuwa hali ya maisha haijabadilika hawazingatii hatua ambayo nchi imepiga, akiwataka wananchi kutambua tofauti iliyopo kati ya hali ya sasa na miaka iliyopita.

Amefafanua kuwa CCM itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera na Ilani yake kwa lengo la kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaambatana na ongezeko la kipato, ajira na fursa za kiuchumi kwa wananchi.