Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi, wageni mbalimbali pamoja na wananchi waliohudhuria hafla ya Uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2115 katika eneo la Rufiji mkoani Pwani tarehe 22 Agosti, 2026.

…………… 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za serikali kujiandaa mapema kukabiliana na mvua kubwa zinazotabiriwa nchini, ili kuepusha maafa na madhara kwa wananchi.

Rais Samia amesema taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zinaeleza uwezekano wa kuwepo kwa mvua kubwa zinazohusishwa na hali ya El Niño, hivyo viongozi wanapaswa kuchukua hatua za tahadhari mapema.

“Niwaombe nendeni mkajitayarishe, mkaweke mazingira sawa ili mvua hizo zitakapoanza zisilete maafa makubwa kwa wananchi wetu,” amesema.

Amesema tahadhari ambazo TMA imeanza kutoa zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito na viongozi kuhakikisha mazingira yanaandaliwa ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.

“Kwa hiyo niwaombe sana, tahadhari zimeanza kutolewa, hatua zichukuliwe ili mvua hizi zisilete madhara kwa wananchi wetu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Agosti 22, 2026, wakati akizungumza na wananchi Mkoani Pwani mara baada ya kuzindua Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Megawati 2,115 wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere.