Na. Meleka Kulwa– Fullshangwe Blog, Dodoma

Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mhe. Anne Makinda, amesema matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa takwimu yanapaswa kuelekezwa katika kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi, badala ya tafiti na taarifa kubaki kwenye machapisho bila kutumika ipasavyo.Ameyasema hayo Agosti 22, 2026 jijini Dodoma, wakati wa hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya NBS, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha (NM-AIST), yenye lengo la kuimarisha matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa takwimu rasmi.

Amesema ushirikiano huo ni jibu muhimu kwa changamoto iliyopo ndani ya NBS, kwa kuwa utawezesha tafiti na taarifa mbalimbali zilizopo kuchakatwa kwa kutumia teknolojia za kisasa na hatimaye kutoa majibu yanayoweza kutumika katika kutatua matatizo ya wananchi.

“MoU hii iliyosainiwa hapa, mimi nafikiri ni jibu kubwa kabisa kwa tatizo letu sisi NBS, Teknolojia iweze kujibu matatizo ya wananchi wa leo,” amesema Mhe. Makinda.

Amesema badala ya tafiti nyingi kuishia kwenye ‘shelves’ bila kutumika ni muhimu taarifa hizo kuingizwa katika mifumo ya kisasa, ikiwemo supercomputer, ili ziweze kuchambuliwa na kuzalisha maarifa yatakayosaidia katika kufanya maamuzi.

Aidha, amebainisha Kuwa NBS imepata fursa kubwa kupitia ushirikiano huo, kwani kuungana na taasisi zenye utaalamu katika sayansi, teknolojia na ubunifu kutaiwezesha taasisi hiyo kupata majibu ya baadhi ya changamoto ambazo imekuwa ikikabiliana nazo.Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, amesema ushirikiano huo utawezesha NBS kuongeza wigo wa upatikanaji wa takwimu rasmi kupitia matumizi ya administrative data na vyanzo visivyo vya kawaida vya takwimu, ikiwemo web scraping.

Aidha, Amesema kuwa NBS  inalenga kuimarisha uwezo wa watumishi wake kupitia mafunzo ya teknolojia na programu mbalimbali, huku ikishirikiana na UDSM na NM-AIST kuhakikisha mafunzo hayo yanaendana na mahitaji halisi ya taasisi.

Amebainisha Kuwa eneo lingine muhimu ni kuimarisha Data Analytics and Statistical Laboratory iliyoanzishwa mwaka wa fedha 2025/26, ili kuongeza uwezo wa wataalamu katika kufanya uchambuzi na kutengeneza ubunifu na suluhisho zitakazosaidia kujibu maswali ya watunga sera, wafanyabiashara na wadau wengine.

Amesema kupitia Joint Steering Committee iliyoainishwa katika MoU hiyo, taasisi hizo tatu zitashirikiana kutengeneza innovations na solutions zitakazotoa majibu kwa changamoto mbalimbali za kitaifa kwa wakati.Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha NM-AIST, Prof. Maulilio John Kipanyula, amesema maamuzi makubwa ya taifa hayawezi kujengwa kwa hisia au makisio, bali yanahitaji takwimu sahihi, ushahidi wa kisayansi pamoja na uwezo wa kufanya modeling, simulations na predictions.

Ameongeza Kuwa ushirikiano kati ya NBS, UDSM na NM-AIST una uwezo wa kuchangia moja kwa moja katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kusaidia taifa kupanga na kufanya maamuzi kwa uhakika zaidi.

Utekelezaji wa mpango huo wa miaka mitano unaanza kwa mwaka wa kwanza, ambapo baada ya kukamilika kwa mwaka huo, watafanya mapitio ya mpango huo kabla ya kuandaa mpango wa utekelezaji kwa mwaka unaofuata.