Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kulia), akiagana na Mwakilishi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bi. Jana Bricco, aliyefika kujitambulisha tangu ashike nyadhifa hiyo pamoja na kufanya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya Tanzania na IMF, ambao umedumu kwa miongo kadhaa tangu miaka ya 1960.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), akiongoza kikao chake na Mwakilishi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bi. Jana Bricco (wa kwanza kulia), aliyefika kujitambulisha tangu ashike nyadhifa hiyo pamoja na kufanya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya Tanzania na IMF, ambao umedumu kwa miongo kadhaa tangu miaka ya 1960.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa kikao chake na Mwakilishi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bi. Jana Bricco (hayupo pichani), aliyefika kujitambulisha tangu ashike nyadhifa hiyo pamoja na kufanya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo alilishukuru Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) kwa mchango wake kwa Tanzania tangu kuanza kwa ushirikiano kati yake na Shirika hilo, akieleza kuwa ushirikiano huo umeendelea kuwa muhimu katika kuimarisha uchumi na utekelezaji wa ajenda za maendeleo nchini.

Mwakilishi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF nchini Tanzania, Bi. Jana Bricco, akizungumza wakati wa kikao na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo aliipongeza Tanzania kwa kukamilisha kwa mafanikio Mpango wa Extended Credit Facility (ECF) inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii na Resilience and Sustainability Facility (RSF) ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, mafanikio ambayo yamechangiwa na kuimarika kwa utulivu wa uchumi jumla, uendelevu wa bajeti na kupungua kwa kiwango cha deni la Taifa.

Kaimu Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Nsubili Joshua (Kulia), Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule (katikati), na Kamishna Msaidizi Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. Juma Mkabakuli, wakifuatilia kikao cha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) na Mwakilishi mpya wa IMF nchini Tanzania, Bi. Jana Bricco (hawapo pichani). (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)

………….

Na. Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amelishukuru Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa mchango wake kwa Tanzania tangu kuanza kwa ushirikiano kati yake na Shirika hilo, akieleza kuwa ushirikiano huo umeendelea kuwa muhimu katika kuimarisha uchumi na utekelezaji wa ajenda za maendeleo nchini.

Ametoa Shukran hizo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi mpya wa IMF nchini Tanzania, Bi. Jana Bricco, ambaye ameanza rasmi majukumu yake nchini, ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya Tanzania na IMF, ambao umedumu kwa zaidi ya miongo sita tangu uanzishwe miaka ya 1960.

Mhe. Balozi Omar amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na IMF katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya Tanzania, ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na mwelekeo wa kimkakati wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaofuata ambayo ni maeneo yenye manufaa kwa pande zote na yanayochangia utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Tanzania.

“Tumekuwa na ushirikiano na IMF kwa muda mrefu, tangu miaka ya 1960 hadi leo, na tumeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali yanayolenga kuimarisha uchumi wa nchi na kufanikisha ajenda yetu ya maendeleo,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aliongeza kuwa Tanzania inathamini ushirikiano huo, hususan katika kufuatilia mwenendo wa ukuaji wa uchumi, sera za fedha na sera za kiuchumi (monetary policy na fiscal policy), pamoja na matokeo ya utekelezaji wa sera hizo.

Mhe. Balozi Omar alisema wataendelea kutazamia kwa pamoja maendeleo ya sekta binafsi na mwenendo wa bei za bidhaa na huduma, ikiwemo mfumuko wa bei (inflation), maeneo ambayo yameendelea kuwa sehemu muhimu ya majadiliano kati ya Tanzania na IMF.

Aidha, Mhe. Balozi Omar ametoa wito kwa Mwakilishi huyo mpya wa IMF kutembelea maeneo mbalimbali nchini ili kupata fursa ya kujionea kwa vitendo maendeleo yanayotekelezwa na Serikali, hususan miradi mikubwa ya kimkakati, kama vile Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere.

“Mbali na miradi ya kimkakati, nakukaribisha kutembelea maeneo ya utalii na uzalishaji, hususan katika sekta ya kilimo na maeneo mengine yenye mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi nchini, na zitakusaidia kupata uelewa mpana zaidi kuhusu fursa, maendeleo na changamoto zilizopo nchini, hivyo kuwezesha majadiliano na ushirikiano wenye tija zaidi kati ya Tanzania na IMF.” alisema Mhe. Balozi Omar

Kwa Upande wake Mwakilishi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bi. Jana Bricco, ameipongeza Tanzania kwa kukamilisha kwa mafanikio Mpango wa Extended Credit Facility (ECF) inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii na Resilience and Sustainability Facility (RSF) ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, mafanikio ambayo yamechangiwa na kuimarika kwa utulivu wa uchumi jumla, uendelevu wa bajeti na kupungua kwa kiwango cha deni la Taifa.

Bi. Bricco amesema mafanikio hayo yalibainishwa na kuthaminiwa katika kikao cha Bodi ya IMF, na kukamilika kwa programu hiyo kunatoa fursa ya kuanza ukurasa mpya katika uhusiano kati ya Tanzania na IMF, utakaojikita zaidi katika mashauriano ya sera, ufuatiliaji wa uchumi na kujenga uwezo wa kitaalamu

“Kukamilika kwa ECF-RSF hakumaanishi mwisho wa ushirikiano kati ya Tanzania na IMF, bali ni fursa ya kuubadilisha na kuuimarisha uhusiano huo kulingana na hatua mpya ya maendeleo ya Tanzania, huku IMF ikiendelea kuwa mshirika katika juhudi za kuimarisha ustawi wa uchumi, uendelevu wa sera na kufanikisha matarajio ya maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2050” alisema Bi. Bricco.

Aliongeza kuwa IMF iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kipindi kijacho kwa kutoa ushauri wa sera unaoendana na mahitaji ya nchi pamoja na msaada wa kujenga uwezo katika maeneo yatakayopewa kipaumbele katika utekelezajinwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“IMF inaona nafasi kubwa ya kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, malengo na maeneo yaliyolengwa katika programu zilizokamilika yana mwingiliano mkubwa na matarajio ya Tanzania ya kujenga uchumi imara, shindani na wenye uwezo wa kutoa fursa zaidi kwa wananchi” alisema Bi. Bricco

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kaimu Katibu Mkuu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Nsubili Joshua, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule, Kamishna Msaidizi Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. Juma Mkabakuli na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na IMF.