Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MADIWANI, watumishi na baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanashiriki kwa wingi mbio za Manyara Tanzanite Marathon 2026 zinazotarajia kufanyika mjini Babati.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kaleya Melita Mollel akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani amesema wamejipanga ipasavyo kushiriki mbio hizo.
Kaleya amesema kwamba wao kwa nafasi yao ya udiwani wamejipanga kushiriki mbio hizo zitakazofanyika Agosti, 22 mwaka 2026 kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa.
Amesema watashiriki mbio hizo zenye lengo la kukusanya fedha za kuboresha huduma za kitengo cha uangalizi na matibabu maalum watoto wachanga hasa wanaozaliwa kabla ya muda au wenye matatizo yanayohitaji uangalizi wa karibu.
“Simanjiro tupo vizuri kwenye mbio hizo, madiwani tumejipanga kukimbia kilometa tano, 10, 21 na 42 bila wasiwasi wowote ule,” amesema Kaleya.
Amesema waratibu wa zoezi wamejipanga vyema kwani kutakuwa na magari yatakayopita njia mbili ya mji mdogo wa Mirerani na barabara ya kata ya Naberera.
Diwani wa kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Maridadi) amesema watu wengi Simanjiro wameitikia mwito wa kushiriki mbio hizo ili kusaidia watoto wa mkoa wa Manyara.
Diwani wa kata ya Mirerani Salome Nelson Mnyawi ameeleza kuwa yeye binafsi atakimbia kilomita tano kwa ajili ya kuunga mkono tukio hilo la kusaidia watoto wa Manyara.
Diwani wa kata ya Ngorika Albert Msole amesema ameshajiandikisha kukimbia kilometa 10 katika mbio hizo za Manyara Tanzanite Marathon 2026.
Mdau wa maendeleo wa mkoa huo, Taiko Kulunju Ole Tipa amesema wao wamejipanga kushiriki mbio hizo ili kumuunga mkono Mkuu wa Mkoa huo Queen Cuthbert Sendiga katika kuwasadia watoto.
