Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa zina nafasi kubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha uwezo wa viongozi na watendaji kuanzia ngazi ya kata hadi vijiji.

 Ameyasema hayo Agosti 21, 2026 jijini Dodoma wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 16 wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), uliolenga kubadilishana uzoefu na mbinu bora za uongozi, kujenga uwezo wa viongozi na watendaji pamoja na kujadili maboresho ya kisera na kiutendaji katika Serikali za Mitaa. 

Aidha,  amesema kuwa Dira ya Taifa ya 2050 si jukumu la Serikali Kuu pekee, bali inahitaji ushiriki wa Mikoa, Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa, akisisitiza kuwa viongozi na watendaji wanapaswa kuchukua maazimio na maarifa waliyoyapata katika mkutano huo na kuyafanyia kazi katika maeneo yao. 

Aidha, amewataka viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa kuepuka migogoro katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza umuhimu wa kuheshimiana na kutambua mipaka ya mamlaka ya kila kiongozi ili kuweka mazingira mazuri ya kazi na kuharakisha maendeleo ya wananchi. 

Aidha, amewataka viongozi hao kuendelea kusimamia matumizi bora ya fedha za Serikali Kuu na mapato ya ndani, pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma bora unaozingatia mahitaji halisi ya wananchi, akisisitiza kuwa Serikali ipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi walioiweka madarakani. 

Amesisitiza kuwa Tanzania ya mwaka 2050 inaanza kujengwa kupitia maamuzi na utekelezaji wa majukumu unaofanyika leo, hivyo viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa wanapaswa kwenda katika maeneo yao ya kazi wakiwa na hatua za utekelezaji, badala ya kurejea na kumbukumbu za mkutano pekee.

 Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), Bw. Albert Msovela, amesema katiba ya taasisi hiyo imefanyiwa marekebisho na sasa Makatibu Tawala wa Wilaya (DAS) wamekuwa sehemu ya wajumbe wa TOA, hatua iliyowezesha ushiriki wao kwa mara ya kwanza katika Mkutano Mkuu wa 16 wa taasisi hiyo.

 

Amesema mkutano huo umejikita katika kauli mbiu inayohusu “ugatuzi wa madaraka kama nyenzo ya kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050”, huku TOA ikiahidi kusimamia maazimio yatakayofikiwa, ikiwemo usimamizi wa rasilimali za umma, watumishi, sheria na taratibu, ukusanyaji wa mapato na uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa wananchi. 

Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kutoa msukumo katika utekelezaji wa sera ya D-by-D (Deconcentration by Decentralization) hadi kukamilika, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha Serikali za Mitaa na kuwezesha utekelezaji wa malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya 2050.