Msanii wa mziki wa kizazi kipya (Bongo Flavour) Q Nchilla akinawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni, ikiwa ni sehemu ya utoaji Elimu juu ya njia za kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona kutoka timu ya uhamasishaji Wizara ya Afya.
Madereva boda boda katika eneo la Studio Dar es Salaam wakifuatilia Elimu juu ya njia za kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona kutoka timu ya uhamasishaji Wizara ya Afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni, au kutumia vitakasa mikono (sanitizer) na kuepuka msongamano isiyo na ulazima.
Mkazi wa eneo la Studio Dar es Salaam akniawa Mikono kwa sabuni na maji tiririka kwa kufuata maelekezo ya Wataalamu kutoka Wizara ya Afya (hawapo kwenye picha).
Eneo la Studio Jijini Dar es Salaam ambapo ni moja ya sehemu ambayo Elimu juu ya njia za kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona imetolewa kutoka kwa timu ya uhamasishaji Wizara ya Afya.
Bara bara inayotokea Tandale darajani Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni moja ya sehemu ambayo Elimu juu ya njia za kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona imetolewa kutoka kwa timu ya uhamasishaji Wizara ya Afya.
………………………………………………………….
Na WAMJW- DSM
Serikali yawaasa wananchi kupata taarifa/habari kupitia vyanzo sahihi ikiwemo Wataalamu wa Afya walioteuliwa kutoa taarifa, tovuti ya Wizara ya Afya na Mitandao ya Kijamii ya Wizara ya Afya ili kuepusha upotoshwaji wa aina yoyote hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya Corona.
Wito huo ameutoa, Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona
“Ndugu zangu, kumekuwa na upotoshaji wa taarifa juu ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona , wito wangu kwenu ni kupata taarifa hizi kupitia vyanzo vinavyotambulika, wakiwemo Wataalamu walioteuliwa na Wizara ya Afya, tovuti ya Wizara ya Afya na mitandao ya kijamii ya Wizara ya Afya ” alisema
Aidha, Ndg. Anyitike Mwakitalima amedai kuwa, kila dereva na kondakta wake ni lazima wahakikishe gari zao zina vyombo vya kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka au kuwa na vitakasa mikono (sanitizer) ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Corona kuendelea kusambaa.
Nae Afisakutoka jeshi polisi kitengo chaushrikishaji jamii Stafu Sajenti Valentino Ngowi, amewaagiza madereva na makondakta wao kuhakikisha kila siku jioni wakimaliza kazi zao wahakikishe wanasafisha magari yao kwa dawa maalum aina ya jiki, ili kuua virusi vinavyoweza kuwepo na kupelekea maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
“Madereva na makondakta wote kila siku jioni, hakikisha jioni mnasafisha magari yenu kwa dawa maalum, wote mnaifahamu jiki hapa, jiki inatumika Kutakasa magari, bajaji au pikipiki ” alisema.
Nae, Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amesisitiza kuwa ili kupambana na ugonjwa huu watu wasichoke kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ili kuepuka kupata maambukizi ya virusi vya Corona.
“Watu wengi wanasema, mimi nilinawa asubuhi kwanini ninawe tena mchana na jioni, tunasema nawa mara nyingi iwezekanavyo, kwasababu mikono ni moja ya sehemu ambayo virusi hivi hupitia kabla ya kuingia ndani ya mwili ” alisema.
Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam.